Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Balozi Hussein Kattanga, akizungumza na Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa ambapo Tanzania inatarajia kuwasilisha Taarifa ya Mapitio ya Hiari ya Nchi ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs), Jijini New York, Marekani. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga na kulia ni Afisa wa Ubalozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa Bw. Joseph Mwasota.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akizungumza Jambo katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania-New York, Marekani, ambapo Tanzania inatarajia kuwasilisha Taarifa ya Mapitio ya Hiari ya Nchi ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs), kwenye Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa. Katikati ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania-Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Balozi Hussein Kattanga, na kulia ni Afisa wa Ubalozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa Bw. Joseph Mwasota.
Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania wanaoshiriki Mkutano wa Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa, wakipata taarifa ya Ushiriki wa Tanzania katika Ubalozi wa Tanzania, Jijini New York Marekani, ambapo Tanzania inatarajia kuwasilisha Taarifa ya Mapitio ya Hiari ya Nchi ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs).
Kamishna Msaidizi wa Idara ya Mipango ya Kitaifa, Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Muhajir Kachwamba (kulia) na Kamishna wa Ardhi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Nathaniel Nhonge, wakipitia taarifa kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Jukwaa la Juu la Siasa ambapo Tanzania inatarajia kuwasilisha Taarifa ya Mapitio ya Hiari ya Nchi ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs), kwenye Jukwaa hilo, Jijini New York Marekani
……..
Na Benny Mwaipaja, New York
Tanzania inatarajia kuwasilisha Taarifa ya Mapitio ya Hiari ya Nchi ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, katika Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa, tarehe 18 Julai 2023, wakati wa mikutano ya Jukwaa hilo iliyoanza jana, Jijini New York, Marekani.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Balozi Hussein Kattanga, alieleza kuwa hii itakuwa mara ya pili kwa Tanzania kuwasilisha Taarifa kama hiyo ambapo mara ya kwanza ilifanya hivyo mwaka 2019.
Alieleza kuwa Jukwaa hilo la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa, ni muhimu kwa kuwa Tanzania itapata fursa ya kueleza fursa na changamoto iliyokumbana nazo wakati wa utekelezaji wa Malengo 17 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu na kupata uzoefu kutoka nchi nyingine 39 zitakazowasilisha taarifa hiyo.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi 39 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizopata fursa hiyo na itatumia nafasi hiyo kubadilishana uzoefu na nchi nyingine zinazoshiriki mkutano huu muhimu” Alisema Mhe. Balozi Kattanga
Alisema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii na kwamba itatumia jukwaa hilo kueleza namna ilivyofanikiwa kupiga hatua za maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo, elimu, afya, maji, amani na usalama wa nchi.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba atawasilisha Taarifa hiyo kwa niaba ya Serikali mbele ya Jukwaa hilo ambapo itajadiliwa na kutoa mapendekezo ya namna ya kufanikisha agenda hiyo ya maendeleo ifikapo mwaka 2030 ambapo mambo kadhaa yanatakiwa kufikiwa ikiwemo kupiga vita umasikini, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, matumizi ya teknolojia, ujenzi wa miji salama, usawa wa kijinsia na mambo mengine kadha wa kadha.