Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan
……..
Julieth Laizer, Arusha.
Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu Hassan ametaja maeneo yanayoongoza kwa rushwa nchini kuwa ni Wanasiasa ,vyombo vya ulinzi na usalama ,ofisi za umma , mahakama ,wafanyabiashara na vyuo vya elimu ya juu huku akiziagiza mamlaka husika kuzifuatilia taasisi hizo.
Ameyasema hayo jijini Arusha katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kupambana na rushwa barani Afrika yaliyoenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 tangu kusainiwa mkataba wa Umoja wa Afrika wa kupambana na rushwa 2003.
Amesema kuwa, swala la kudhibiti rushwa ni jambo la kila mmoja wetu kila mmoja kuhakikisha wanakemea na kupinga vitendo vya rushwa kwani rushwa ni adui wa haki.
“Watu waliosemwa sana ni sisi Wanasiasa,Wafanyabiashara lakini Maofisini nako kumelaumiwa halikadhalika mahakamani nako hakukunusurika hivyo washiriki wa maadhimisho hayo tumeshuhudia na wale wote waliohusika katika maeneo haya kufuatilia maadhimio ya mkutano huu na twende tukafanye marekebisho,”alisema Rais Samia.
Rais Samia amesema ni vyema kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anafanya juhudi katika kupambana na kuzuia na kupambana na rushwa kwa hiyo ni rai yake wa wadau mbalimbali kujitafakari kwa lengo la kubainisha changamoto na vikazo vya mapambano hayo.
Ameongeza kuwa, Tanzania ilisaini mkataba huo tarehe 5,novemba 2003 na kuridhia 22 febuari 2005 na tulianza kuutumia mkataba huo rasmi tarehe 5 agosti 2006 na Tanzania ni miongoni mwa nchi 48 kati ya nchi 55 zilizosaini na kuridhia mkataba huo na tumekuwa tukiadhimisha siku hii tangu mwaka 2018.
Mkurugenzi Mkuu wa kuzuia na kupambana na rushwa nchini CP Salum Hamduni amesema katika kuadhimisha siku hiyo ya madawa ya kulevya imeenda sambamba na kongamano ambalo lililenga kutoa elimu kuhusu swala la maadili,utawala bora,na elimu namna ya kupinga na kupambana na rushwa na uhujumu uchumi.
Ameongeza katika kongamano hilo ilitolewa elimu kuhusu maswala ya utalii nchini na kuweza kupata uzoefu kutoka nchi mbalimbali .
Naye Waziri wa nchi ofisi ya Rais katiba sheria utumishi ,utawala bora wa serikali ya mapinduzi Zanzibar ,Harun Ali Suleman amesema kuwa,wameweza kupata uzoefu zaidi kutoka nchi mbalimbali namna zinavyofanya kazi ikiwemo nchi ya Singapore na Hongkong kwani ni moja ya nchi ambazo zimefanya vizuri ,hivyo ni vizuri na nchi ya Tanzania ikaenda kujifunza zaidi katika nchi hizo.
Kwa upande wake Waziri ofisi ya Rais menenejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora ,George Simbachawene amesema kuwa, siku ya kilele cha kupinga siku ya kupambana na madawa ya kulevya wameweza kujadili maswala mbalimbali ikiwemo uzoefu wa Mahakama katika kupinga na kupambana na rushwa barani Afrika.
“Tanzania tumepewa heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa mkutano huu ambao ni tukio muhimu sana ,na hivyo tunaahidi kuendelea kusimamia taasisi za kupambana na rushwa katika nchi yetu Tanzania bara na visiwani,”amesema ,Simbachawene