Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma, Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Umma Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani wakati wa muendelezo wa ziara yake ya siku tano mkoa Pwani
……..
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha, Julai 11
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma, Ridhiwani Kikwete amewaagiza maofisa Utumishi kutenda haki kwa watumishi pamoja na kusimamia maelekezo na maagizo yote wanayokuwa wakipatiwa ngazi za juu.
Hatua hiyo itasaidia kupunguza kuzalisha changamoto za watumishi na kupunguza malalamiko yanayojitokeza kwenye utendaji wa kazi yao.
Akizungumza na watumishi wa Umma Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani wakati wa muendelezo wa ziara yake ya siku tano mkoa Pwani, Ridhiwani aliwaasa maofisa hao kutimiza wajibu wao.
“Mnafaidika nini kama mkikaa bila kushughulikia matatizo ya watumishi,kuwaongeza vyeo, kulipa malimbikizo au kushughulikia malimbikizo ya watumishi,mnakuwaje na uchungu wa fedha ambazo zinatolewa na Serikali kulipa stahiki za watu,Tendeni haki kwa fedha za Serikali na kufanyia kazi maelekezo yake”alieleza Ridhiwani.
Aidha aliwataka , Maofisa Tawala wawe viungo kwa mamlaka za ajira.
Maagizo hayo aliyatoa baada ya kufikishiwa malalamiko dhidi ya ofisi ya Utumishi Halmashauri ya wilaya ya Kibaha, ikiwemo malimbikizo ya mshahara ya muda mrefu, watumishi kutopandishwa madaraja muda mrefu,na watumishi wanaokwenda kuongeza elimu kupunguziwa mshahara.
Kufuatia malalamiko hayo, Ridhiwani alimuagiza ofisa Utumishi wa Halmashauri hiyo, Edward Masona kuhakikisha anashughulikia changamoto zote alizozikuta katika ofisi hiyo.
Alimtaka aende kwenye maeneo yote kuanzia Ngazi ya chini yaliyo kwenye eneo lake la kazi kuzungumza nao, kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitatua.
Ridhiwani alisema, changamoto ambazo zitakuwa nje ya uwezo wake aziandikie barua kwa Katibu Mkuu wizara ya Utumishi ili asaidiwe atakapokwama .
“Nyumba uliyoikuta ni mbaya, kwakuwa umekuta changamoto za kipindi kirefu ambazo hazijatatuliwa, haiwezekani watu wanadai malimbikizo toka 2014″alisisitiza Ridhiwani.
“Mtu katoka kufanya kazi magazetini leo kaletwa Halmashauri kitengo cha manunuzi,unakaa nae hujui kama una mtu wa aina hiyo asiye kwenye kada yake “jirekebishe Fanyieni kazi malalamiko yote yaliyopo mezani.
Ndalahwa Butamo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha, alieleza ,kuna mahitaji 2012 ya watumishi, waliopo 1,571 upungufu ni 441.
“Kwa mwaka 2023/2024 tumetenga bajeti ili kuajiri watumishi 211″Lakini pia uhaba mkubwa wa watumishi upo idara ya Utumishi na utawala 140 waliopo 80″alieleza Butamo.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo alitaka suala la uhamisho liwekewe Utaratibu ili kuondoa manung’uniko.
Kuhusu uhaba wa nyumba za watumishi na wastaafu kustaafu bila Kuwa na makazi bora, Mwakamo alishauri wizara kufanya mpango wa kuzungumza na mashirika ya nyumba kuangalia uwezekano wa kujenga nyumba za watumishi kwa Utaratibu watakaoona unafaa.