Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga akizungumza kuhusu kukamatwa kwa kadi zaidi ya 1300 zinazotumikakinyume cha utaratibu wa bima ya afya.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakuu wa idara katika shirika hilo.
…………………………………..
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF umechukua hatua mbalimbali ikiwemo kusitisha matumizi ya kadi za wanachama 697, kuamuriwa kulipa gharama za matibabu zilizotumika 325, kuwafungulia mashtaka 67 na kuwaripoti katika Mamlaka za uchunguzi 108, kufuatia kukamatwa kwa takribani kadi 1,346 ndani ya kipindi cha Mwaka mmoja zikitumika na watu wasio wanachama.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo amesema zoezi hilo awali lilianza Juni Mosi mwaka huu.
Konga amesema kwamba waliingia kwenye vituo vya kutolea huduma ambavyo wana mkataba navyo ambapo walianza na mikoa sita ya Dar es Salaam,Mbeya,Mwanza,Arusha,Kilimanjaro na Dodoma.
Ameongeza kwamba katika operesheni hiyo wamebaini mapungufu mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya kadi ambazo zimebainika kutumiwa na watu ambao si wanachama wa mfuko huo kinyume na taratibu.
Amesema mfuko pia umebaini wanachama 2,490 wameacha kadi zao vituoni ambapo kwa sasa wanachunguza sababu za kutelekezwa kwa kadi hizo.
“Mbali na kadi hizo kutelekezwa pia tumebaini wanachana 1,346 wameazimana kadi ambapo wakaguzi wamezikamata na kuanza kuchukua hatua zinazostahiki kulingana na taratibu.
Amesema mbali na kuzikamata kadi hizo, uchambuzi unafanyika kubaini gharama zilizotumika kuhudumia watu wasio wanachama kwa kutumia kadi hizo.
Ametanabaisha kuwa kufanya hivyo ni kinyume na utaratibu wa sheria na endapo yeyote atakayebainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Amesema uchunguzi unaendelea kufanyika kubaini imewezekanaje watoa huduma kushindwa kutambua wasio wanachama wanaotumia kadi za wanachama.
Aidha amesema uhakiki huo ndani ya mwezi mmoja umebaini wanachama 2,490 wameacha kadi zao vituoni.
“Tunaendelea kuchunguza ili kujua je, mtoa huduma amemtaka mwanachama aache kadi ili baadae atengeneze dai, au mwanachama ameisahau,” amesisitiza.