Afisa Usajili Chuo Cha Bandari Dar es Salaam Bw. Mosses File akiwataka watanzania kuchangamkia fursa ya kujiunga na chuo cha Bandari kwa ajili ya masomo mbalimbali yakiwemo ueneshaji wamitambo ambapo vigezo ni mtu kuwa na leseni tu inatosha kujiunga na mafunzo.
…………………………….
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa kwa kusoma kozi mbalimbali zinazotolewa na Chuo cha Bandari ya Dar es Salaam jambo ambalo litawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi katika shughuli za bandari.
Akizungumza katika maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea Jijini Dar es Salaam, Afisa Usajili Chuo Cha Bandari Dar es Salaam Bw. Mosses File, amesema kuwa Chuo kinatoa ushauri pamoja na kufanya utafiti.
Bw. File amesema kuna mafunzo ya uendeshaji wa mitambo ambapo mwanafunzi baada ya kuhitimu masomo yake anakwenda kufanya kazi bandarini au taasisi ambayo shughuli zake zinafanana na bandari.
Amesema kuwa katika kozi uendeshaji mitambo mwanafunzi atafundishwa namna ya kuendesha mashine katika kipindi cha muda wa wiki sita,
“Sifa ya kusoma kozi ya uendeshaji wa mitambo wanafunzi anatakiwa kuwa na leseni ya udereva kuanzia daraja D” amesema
Amebainisha kuwa pia wanatoa programu ya utekelezaji wa shughuli za mali na bandari ambapo wanakwenda kuwa makarani wa bandari katika kuhakikisha shughuli zinakwenda sawa.
Kozi nyengine wanazotoa ni pamoja na usafirishaji ndani ya maji, usimamizi na utengenezaji wa vifaa vyote ambavyo vipo baharini.