Na Mwandishi wetu, Mirerani
WACHIMBAJI wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani, Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kuwatumia wataalamu wa miamba na kufanya utafiti kwenye maeneo wanayochimba ili kuepuka migogoro na mitobozanno na kitalu C.
Meneja mkuu wa kampuni ya Franone Mining LTD, Vitus Ndakize akizungumza mbele ya Waziri wa Madini, Dotto Biteko alipotembelea kitalu C, amesema baadhi ya wachimbaji wana dhana potofu kuwa madini ya Tanzanite yapo kitalu C pekee.
Ndakize amesema baadhi ya wachimbaji wa madini ya Tanzanite, badala ya kuwatumia wajiolojia, wao wana dhana potofu kuwa mashapo ya madini yapo eneo la kitalu C pekee, suala ambapo siyo kweli.
“Wanatakiwa kutumia gharama kufanya utafiti kwa kupitia wataalamu wa miamba, ambao hivi sasa wapo wengi tuu kuliko miaka iliyopita, ila wanatumia gharama kubwa kulipua baruti kwenye miamba hivyo kupoteza fedha zao,” amesema.
Amesema baadhi ya wachimbaji wa madini ya Tanzanite, waliopakana na kitalu C, wanatobozana nao na kusababisha migogoro isiyo na tija kwa kufuata njia zao badala ya kuwatumia wataalamu wa miamba wakihofia gharama.
Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining LTD, Onesmo Mbise amesema ombi la mabroka kutaka kuuziwa madini ya Tanzanite linapaswa kusubiri tamko la Serikali kuruhusu minada.
Onee amesema endapo kukiwa na minada kutakuwa na utaratibu mzuri ulioandaliwa na Serikali ili awamu ya wanunuzi wadogo na wakubwa upangwe hivyo wasubirie.
“Ila kwa sasa huwezi kupeleka madini eneo la Opec ‘kitalu B’ au kitalu D useme unawafuata mabroka kutaka kuwauzia madini ya Tanzanite kabla Serikali haifaandaa utaratibu wa minada,” amesema Onee.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Money Yusuf amesema ni dhana potofu kudhani madini ya Tanzanite yanapatikana pekee.
Amesema madini ya Tanzanite yanachimbwa kwa kufuata mkondo na madini yenye rangi nzuri, yasiyo na kasoro na yenye umbo na suru ya in kuvutia yapo kitalu D na Karo, na kutoa mfano kuwa unaweza kupata jiwe la Tanzanite kwenye kitalu B na kuyaweka jioni ila kesho yake asubuhi ukalikuta limevunjika inabidi uliweke kwenye jokofu.
“Justin Nyari alipata madini mazuri mno kwenye mgodi wake namba sita kipindi kile alivumbua Block D na watu wakakimbilia jirani yake baada ya yeye kuepuka vurugu kule Opec,” amesema Money.
Amesema hata yeye binafsi mara ya mwisho alipopata madini kwenye mgodi wake ‘mbuzi mawe’ uliopo kitalu D alikwenda kuyauza baadhi Marekani na kupata kiasi kikubwa cha fedha, kutokana na uzuri wa madini hayo.
“Kwa gharama zangu nilivuta nishati ya umeme kwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 30 na kuufikisha kitalu D bila kutegemea Serikali na umeme huo bado unatumika na wachimbaji hadi hivi sasa,” amesema Money.
Amesema wachimbaji wadogo wameshachangia kiasi kikubwa cha maendeleo ya jamii mji mdogo wa Mirerani, ikiwemo kujenga kituo cha polisi, sekondari na kuvuta umeme kutoka Kia hadi Mirerani.
Hata hivyo, Waziri wa Madini Dotto Biteko amewaasa wachimbaji madini kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari ili waweze kujulikana kuwa wamechangia maendeleo kwa jamii.
“Sasa wewe unajenga madarasa, unachimba kisima cha maji au kusaidia zahanati, kituo cha afya au hospitali kwa kufanya kimya kimya kasha unataka jamii ikutambue kuwa umechangia maendeleo?” amehoji Waziri Biteko.