Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala Mhe. Mohamed Ramadhani Msofe akikabidhi kadi za Jumuiya ya Wazazi kwa viongozi matawi na mashina Kata ya Mzinga.
Wanachama wa Jumuiya ya Wazazi CCM Kata ya Mzinga wakiwa katika kikao kazi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala Mhe. Mohamed Ramadhani Msofe tarehe 8/7/2023
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ialla leo tarehe 8/7/2023 wameendelea na ziara katika Kata ya Mzinga kwa ajili ya kuangalia uhai wa jumuiya kuanzia ngazi ya matawi pamoja mashina.
Akizungumza na Wanachama wa Jumuiya ya Wazazi CCM Kata ya Mzinga, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Wilaya ya Ilala Mhe. Mohamed Ramadhani Msofe, amewataka viongozi wa matawi na mashina kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta tija na kufanikiwa kusonga mbele ikiwepo kuondoa dhana iliyojengeka Kuwa Jumuiya ya Wazazi ni Jumuiya ya Wazee.
Mhe. Msofe pia amegawa kadi 50 za Jumuiya ya Wazazi kwa kila tawi, huku akiwataka kutumia kadi hizo sehemu ya mtaji kwa kujipatia kipato kwa kuwauzia Wananchi ili kuweza kushawishi kujiunga na Jumuiya ya Wazazi kuwa wanachama.
“Mkiuza leteni ripoti kwa Katibu Kata na Katibu Kata wa Wazazi Kuleta ripoti Wilayani ili awape kadi nyengine baada ya miezi mitatu tutarudi tena, nendeni mkatoe kadi na kuongeza wanachama” amesema Mhe. Msofe.
Katika ziara hiyo Mhe. Msofe ameongozana na kamati ya utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya iIala katika kuhakikisha wanatoa elimu pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Aidha amewaelekeza zipo baadhi ya Changamoto anazipokea na kuziwasilisha kamati ya siasa Wilaya ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwani jumuiya hiyo ipo chini ya Chama cha Mapinduzi.
Kupitia maelezo hayo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Mzinga alimshukuru Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya yeye na timu yake ya kamati ya utekelezaji Wazazi Wilaya kwa kuja kutembelea Kata yake na kujionea hali halisi ya mshikamano.