Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Hassan Abbasi amewakaribisha wananchi na wadau mbalimbali kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana kwenye hifadhi za misitu ya Serikali nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere maarufu sabasaba alipotembelea maonesho ya 47 ya kimataifa ya Dar es salaam leo tarehe 08/07/2023 kuona namna Wizara ya Maliasili na Utalii inavyoshiriki katika maonesho hayo.
Dkt Abbasi amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imejikita katika kubuni fursa mbalimbali zinazolenga kumkwamua mwananchi hasa kwenye maeneo ya uwekezaji katika sekta ya Utalii, misitu na malikale.
“Serikali inapanga mikakati mingi kuongeza fursa kwenye maeneo ya uhifadhi na tayari wataalamu wetu wanaandaa mkakati mmojawapo unaoitwa “achia shoka kamata mzinga” maana yake uache kukata miti ili utundike mizinga ufuge nyuki,”
“Pamoja na kwamba elimu kwa wananchi haijawa kubwa lakini tayari asali inachangia kwa asilimia kubwa pato la taifa na sasa tunataka hamasa na elimu itolewe zaidi ili kuongeza uwekezaji katika ufugaji nyuki” Amesema Dkt Abbasi.
Ameongeza kuwa kwenye maeneo mengi ya hifadhi za misitu kuna fursa ya kuwekeza kwenye shughuli za utalii hasa ujenzi wa miundombinu na huduma za chakula na malazi na hivyo kuwakaribisha wadau mbalimbali kuchangamkia fursa hizo hasa katika kipindi hiki ambapo utalii umeonesha mafanikio makubwa kutokana na Filamu ya Royal Tour.
Aidha, Dkt Abbasi amepongeza Mamlaka, Wakala na taasisi za Wizara kwa kushiriki maonesho ya 47 ya kimataifa ya biashara ya Dar es salaam ya 2023 huku akisisitiza taasisi hizo kuongeza matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma hasa huduma za utalii.
Naye Kamishna wa uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo ambaye ameambatana na Katibu Mkuu kwenye ziara hiyo amewakaribisha wananchi na wadau kutembelea banda la Maliasili na utalii hususani eneo la TFS ambapo watapata uelewa kuhusu faida za uhifadhi endelevu wa misitu.
“Nitoe wito kwa wananchi na wadau kutembelea maeneo yetu kwenye maonesho haya lakini kuna wengine hawajaweza kufika bado lakini wanaweza kujifunza kupitia vyombo vya habari ambavyo tumekuwa tukitumia kwenye maonesho haya wapate uelewa kuhusu fursa za uwekezaji kwenye ufugaji nyuki, biashara ya asali, utalii ikolojia, uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu.”
Hata hivyo Prof. Silayo ameendelea kusisitiza utunzaji wa misitu yote nchini ili kuleta matokea chanya ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na kupanda miti kwa wingi na kuhakikisha miti inayopandwa au iliyopo inatunzwa kwaajili ya kizazi cha sasa na cha baadae.
“Kumekuwa na changamoto nyingi kwenye uhifadhi lakini changamoto kubwa ni moto, moto unaharibu sana misitu na hivyo natoa wito pia kwa wananchi kuendelea kushirikiana na aerikali kwa kujiepusha na uanzishaji wa moto holela lakini pia kuudhibiti haraka pale unapozuka,” Amesema Prof. Silayo.
Sambamba na hilo Prof. Silayo amemshukuru Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Hassan Abbas kwa kutenga muda wa kutembelea banda la Maliasili na Utalii na kukutana na wadau walileta vioneshwa kwenye maonesho hayo.
Maonesho ya 47 ya kimataifa ya Dar es salaam(sabasaba 2023)yanaendelea jijini Dar es salaam kwa kauli mbiu isemayo “Tanzania mahali sahihi kwa biashara na uwekezaji” na yanatarajiwa kufungwa tarehe 13/07/2023