Na Beatrice Sanga-MAELEZO
Serikali imesema kuwa itahakikisha inaongeza ufanyaji biashara na nchi ya India pamoja na bara la Asia kwa ujumla katika kilimo, teknolojia viwanda na elimu.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shabaan katika kongamano lililowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka India na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) waliofika na kujionea fursa za uwekezaji zilizopo nchini pamoja na kushiriki na kuhudhuria katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya biashara Maarufu (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja wa Sabasaba, huku akisema kuwa bado ufanyaji biashara kati ya nchi hizo mbili hauko katika mizani ya usawa.
“Ukiangalia hali ya ufanyaji wa biashara kati ya Tanzania na India (Trade balance) bado inawapendelea sana India kwa maana wanaleta bidhaa nyingi zaidi kuliko zile ambazo sisi tunasafirisha, lakini utayari wa viongozi wetu wa kuweka miundombinu mizuri ya uwekezaji hasa katika sekta ya uzalishaji wa viwandani, tunaamini miaka ijayo basi utofauti (Gap) huo wa biashara utapungua, kwasababu uwekezaji wa viwanda umekuwa mwingi hivyo tutakuwa na fursa ya kuzalisha na kusafirisha bidhaa kwenda nje hasa taifa la India ambao wameonesha utayari.” Amesema Waziri Omar
Waziri Omar ameongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya sera za uwekezaji na elimu hususani eneo la teknolojia nchini hasa kufuatia kuanzishwa kwa Kampasi ya chuo Kikuu cha Teknolojia cha Indian Institutes of Techology (IITs) Mjini Zanzibar kutoka India, yatasaidia kuimarisha teknolojia na uzalishaji wa bidhaa kwa njia za kisasa na kuongeza ufanisi katika shughuli za uzalishaji viwandnai, huku akitanabaisha kuwa mazao ya kilimo yataongezeka maradufu katika kuzalishwa na kusafirishwa kuelekea nchini India.
“India ni watumiaji wazuri wa chai, sisi hapa tunalima sana chai, lakini pia zao la karafu na viungo vingine, lakini pia madini pamoja na korosho, India ni watumiaji wazuri wa bidhaa za korosho duniani, tunayo ardhi kubwa tunaweza kuzalisha na kuwapelekea, kwahiyo tunayo fursa kubwa ya kushirikiana na wenzetu katika kuongeza zaidi biashara, hatujatumia fursa ipasavyo bado soko ni kubwa, nchi ya India ni kubwa na ina watu wengi hivyo hatujalitumia vyema soko,” amefafanua Waziri Omar.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Gilead Teri amesema kuwa kutokana na mabadiliko mbalimbali ya sera za biashara, kumaimarika kwa ufanyaji biashara, na uwekezaji yanayofanywa na serikali yamezidi kuwavutia wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza nchini, hivyo jambo hilo linazidi kuongeza fursa za biashara na uwekezaji na kuchochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla na kutoa wito kwa wawekezaji kuendelea kuja kuwekeza hapa nchini.
“Jambo kubwa tunaloliona kwa sasa hivi wawekezaji wengi wanaokuja ni wa daraja la kati (Middle income investors) hawa ni wawekezaji wa muhimu sana kwa nchi yoyote inayotaka kupunguza umaskini, siyo uwekezaji mkubwa tu lakini pia, ni uwekezaji ambao unaweza ukatoa ajira nyingi, ndo uwekezaji tumeupata leo wawekezaji zaidi ya mia moja tumefanya nao mkutano tumewapa taarifa ya fursa zilizopo Tanzania na sisi TIC tumewaeleza ni kwa namna gani tunaweza kuwasaidia wao kuanzisha biashara zao na uwekezaji wao hapa nchini ili uweze kuleta manufaa kwa jamii ya watanzania.”
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya India S. Jaishankar aliyeambatana na ujumbe wake amesema kuwa Tanzania na India wamekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika maeneo mbalimbali ikiwemo, maji, afya, teknolojia, elimu, uwekezaji, diplomasia hivyo nchi hiyo itaendelea kuhakikisha ushirikiano huo unaendelea kukua na kuelta manufaa zaidi kwa nchi zote.
“India ni nchi ya tano kwa ukuaji wa uchumi duniani, hivyo kutokana na Tanzania kuonesha hali nzuri ya ukuaji wa kiuchumi barani Afrika ni dhahiri kuwa tutaongeza maeneo ya uwekezaji na ushirikiano na Tanzania katika maeneo ya biashara na miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema Waziri S. Jaishankar.
Kongamano hilo lilikuwa malengo ya kuwatambulisha wafanyabiashara hayo katika maeneo ya uwekezaji hapa nchini ingawa imeelezwa kuwa wawekezaji waliokuja watarajia kuwekeza zaidi kwenye maeneo ya uchakati wa chakula (Food processing), bidhaa za misitu, (Wood products) lakini pia bidhaa za ujenzi kama vile nondo, cement, chuma, Sekta ya elimu, afya na viuatilifu, pamoja na bidhaa za chanjo.