Dar es salaam
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Mhe. Omary Juma Kipanga (mb) , ametoa wito huo kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuimarisha na kukuza bunifu katika kutatua matatizo yanayoikabili jamii ya Watanzania ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ulimwenguni.
Pia, Mhe Kipanga aliongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu sekta hiyo, kwani imewekeza kiasi kikubwa cha fedha, kuanzia Shilingi Bilioni 3 hadi 9, ili kuimarisha na kuendeleza eneo la ubunifu. Hatua hii inalenga kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali katika sekta tofauti.
Naibu Waziri Kipanga alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipotembelea banda la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) katika maonyesho ya Kimataifa ya biashara ya 47, yaliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba, Wilaya Temeke , Jijini Dar es Salaam.
“Tunatambua kuwa katika miaka michache iliyopita, bajeti yetu katika eneo la ubunifu ilikuwa Shilingi Bilioni 3. Hivyo, kuongezeka kwa sasa kutatusaidia kuendelea kukuza na kutatua changamoto kwa wazalishaji,” alisema Naibu Waziri Kipanga
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt Amosi Nungu, alisema kuwa serikali inasaidia vijana mbalimbali ili waweze kuwekeza na kukuza maendeleo ya nchi.
Aidha, Naibu Waziri Kipanga alihitimisha kwa kusema kuwa Wizara ya Elimu itaunda ushirikiano na Wizara ya Kilimo, kwani vijana wengi wamekuwa wakifanya ubunifu katika kilimo na hivyo kujenga fursa nyingi za ajira.