Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ameanza kuyagusa makundi maalum yasiyojiweza kwa kutoa misaada itakayowasaidia kutatua changamoto zao wilayani Magu mkoani Mwanza .
Hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wa majukumu yake na pia ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Ndugu Mary Chatanda pamoja na Naibu wake Ndugu Zainabu Shomari ya kuwataka viongozi wa Chama cha Mapinduzi kuwa mfano wa kuigwa kwa kuyaangalia makundi maalum yasiyojiweza na kutoa misaada mbalimbali itakayowasaidia kutatua changamoto zao.
Katika kutekeleza agizo hilo Mhe.Masanja ametembea nyumba kwa nyumba na kutoa msaada wa baiskeli tano za walemavu wa miguu zenye thamani ya shilingi milioni 3.2, majiko matano ya gesi yenye thamani ya shilingi laki tatu, fedha taslimu laki moja na nusu kwa kila mhitaji pamoja na kuahidi kuwalipia bima ya afya watoto hao wenye ulemavu katika Tarafa tatu za Wilaya ya Magu ambazo ni Sanjo,Itumbili na Kahangara.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Masanja amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni Serikali ya vitendo na moja ya vitendo ni kutembelea kila jamii kuangalia changamoto za watoto, kinamama na vijana na kuzitatua.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu ni Serikali pekee na Rais pekee itayoweza kuwavusha watanzania kutoka uchumi wa chini mpaka juu.
Naye, Mericiana Faustine ambaye ni miongoni mwa wanufaika wa msaada huo ametumia fursa hiyo kutoa shukrani zake kwa Rais Samia Suluhu Hassan huku akiahidi kuendelea kuiomba Serikali kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum na maeneo mengine
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Magu, Loyce Mabula amewataka Watanzania kumuunga mkono Rais Samia kwa kuwa na viongozi wanaojitolea kutatua matatizo ya watu wenye mahitaji maalum.
Diwani wa Viti Maalum, Mhe. Diana Philemon amemshukuru Mhe. Masanja kutoa misaada hiyo.