Na Ahmed Mahmoud
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Husein Ali Mwinyi anatarajia kuzindua Maadhimisho ya siku ya mapambano dhidi ya Rushwa barani Afrika Mkoani Arusha.
Akiongea na vyombo vya Habari Jijini Arusha Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela Amesema Maadhimisho hayo yatakuwa siku tatu kuanzia Tarehe 9 hadi 11 na siku ya Tarehe 9 Dkt Mwinyi atazindua matembezi ya kupinga Rushwa ikiwa ni ufunguzi wa Maadhimisho.
Alisema Kwa Mgeni Rasmi katika kilele cha Maadhimisho hayo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo kwenye Maadhimisho hayo tunatarajia kwamba wadau mbalimbali wa Ndani na nje ya nchi watashiriki.
Aidha alisema kwamba sanjari na Maadhimisho hayo ya siku ya mapambano dhidi ya Rushwa barani Afrika katika mwaka huu 2023 pia tunaadhimisha miaka 20 ya utekelezaji wa mkataba wa Umoja wa Afrika wa kuzuia na kupambana na Rushwa (AUCPCC) mkataba huo ulisainiwa mwaka 2003.
Kwa mujibu wa Mongela alisema kwamba washiriki wa Mkutano huo ni nchi zote wanachama za Afrika zilizosaini mkataba huo Pamoja na washiriki wengine wanasiasa wawakilishi wa Mabalozi wawakilishi wa Taasisi binafsi viongozi wa dini vyombo vya Habari wajumbe wa AUABC na watumishi wa Sekretarieti ya bodi.
“Ni fahari kubwa Kwetu sisi wakazi wa Mkoa wa Arusha hususani wakazi wa JIJI la Arusha kupata fursa ya kuwapokeaviongozi wakuu wa nchi yetu hivyo tudumishe Amani utulivu na usalama kama ilivyo desturi yetu kama nchi na Mkoa wetu”
Alisema siku ya mapambano dhidi ya Rushwa barani Afrika huadhimishwa julai 11 ya kila mwaka tangia ilipoazimiwa hivyo mwaka 2017 na mwaka huu wa 2023 Tanzania imepewa heshima ya kuwa nchi mwenyeji wa Maadhimisho haya.
Aidha kama ilivyo desturi yetu wakazi wa JIJI la Arusha naomba kuwasihi pia kujitokeza kuwapokea viongozi wetu wakuu na wageni mbalimbali Kutoka mataifa ya Afrika na nje ya bara hili sanjari na wageni wanaotoka mikoa mbalimbali kuja kwenye Maadhimisho hayo.