Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Zanzibar akizungumza leo tarehe 5/6/2023 wakati akifungua Mjadala wa wazi Kuelekea siku ya Kiswahili ambao umejikita kwenye mada inayosema “Kiswahili Nyenzo ya Ukombozi wa Fikra kwa Maendeleo ya Kiuchumi Barani Afrika”.
…….
Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa agizo kwa Baraza la Kiswahili La Taifa na Baraza la Kiswahili Zanzibar kupeleka Wataalam wa Ukalimani katika Taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kukuza na kueneza lugha hiyo.
Mhe. Chana ametoa maagizo hayo leo Julai 5, 2023 Zanzibar wakati akifungua Mjadala wa wazi Kuelekea siku ya Kiswahili ambao umejikita kwenye mada inayosema “Kiswahili Nyenzo ya Ukombozi wa Fikra kwa Maendeleo ya Kiuchumi Barani Afrika”.
“Naipongeza Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa nia ya dhati na kwa mchango walioutoa kushirikiana na Watanzania kwa moyo wao wa dhati kuandaa andiko na kujenga hoja kwa kuonesha ushahidi kwamba Kiswahili si lugha ya Tanzania pekee bali Afrika na Duniani kote” amesema Mhe. Chana.
Aidha, Dkt. Chana ametoa pongezi kwa mabaraza hayo kwa juhudi kubwa wanayoendelea kufanya katika kubidhaisha Kiswahili ndani na nje ya nchi, ambapo mpaka sasa vituo 10 vimefunguliwa katika Balozi za Tanzania katika nchi za Ufaransa, Hispania, Abudhab, Zimbabwe, Korea Kusini, Sudani, Nigeria na Mauritius.
Ameongeza kuwa, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020- 2025 ina malengo ya kukiendeleza Kiswahili, miongoni ni pamoja na Lugha hiyo kutumika kikamilifu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU) ” Balozi Dkt. Pindi Chana – Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Hata hivyo, amezitaka Taasisi za biashara na huduma kutumia lugha ya Kiswahili katika matangazo na mabango ya bidhaa na huduma zao kwa kuwa Watanzania wengi wanatumia lugha ya Kiswahili kuliko lugha za kigeni.