Na. Damian Kunambi, Njombe.
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva amewataka wahudumu wa afya kutoa huduma nzuri na kauli zisizoudhi kwa wagonjwa wanaofika katika hospitali, vituo vya afya pamoja na zahanati mbalimbali kwa lengo la kupata huduma hiyo hata kama watoa huduma hiyo wako wachache na kuzidiwa na wingi wa wagonjwa.
Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo katika mkutano wa uzinduzi wa zahanati ya Mkiu iliyopo katika kata ya Lubonde wilayani humo ambapo zahanati hiyo inaanza kutoa huduma ikiwa na wahudumu wa afya wawili pekee.
“Najua kwa sasa mmeletwa wahudumu wawili tuu kuanza kutoa huduma hapa, kwa idadi yenu najua muda mwingine mnaweza kuzidiwa na wingi wa wagonjwa ambao wote wanategemea huduma yenu, sasa niwaombe mkawe na kauli nzuri kwa wagonjwa na kuwapa huduma stahiki wakati serikali ikiendelea kuona uwezekano wa kuleta wahudumu wengine zaidi”.
Sanjali na hilo mkuu huyo wa wilaya aliwapongeza wananchi kwa kuanzisha ujenzi wa zahanati hiyo na kusema kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imelenga kuwaunga mkono wananchi katika shughuli zote za kimaendeleo.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa zahanati hiyo afusa mtendaji wa kijiji hicho Daniel Henjewele amesema wananchi wamechangia kiasi cha sh. Mil. 22.5, serikali kuu Mil. 50 lakini pia Halmashauri ya wilaya hiyo ilitoa fedha kiasi cha zaidi ya sh. Mil. 29 ambazo zote kwa pamoja zimetumika katika kukamilisha miundombinu ya majengo, ununuzi wa vifaa tiba na kusaliwa na kiasi cha sh. Mil. 10.4.
Stanley Mlay ni mganga mkuu wa wilaya hiyo huduma zitakazotolewa hapa ni huduma za uzazi, matibabu ya wagonjwa wa nje, huduma za chanjo, upimaji virusi vya ukimwi pamoja na matibabu pamoja huduma za ngazi ya jamii ambazo hutolewa kwaajili ya wagonjwa ambao hawana uwezo wa kufika katika zahanati.
Ameongeza kuwa katika kijiji hicho cha Mkiu kuna eneo la barabara ambalo lina mlima mkali na limekuwa likisababisha ajali za mara kwa mara hivyo zahanati hiyo itasaidia kuhudumia kwa haraka wagonjwa wa dharua watakaokuwa wanapatwa na majanga ya ajali za barabarani.