……
Benki ya NMB imetoa msaada wa bati 200 zenye thamani ya shilingi milioni 8,400,000 katika shule ya sekondari Iwawa iliyopo wilayani Makete mkoani Njombe ili kusaidia ujenzi wa bweni la kulala wanafunzi wa kiume.
Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya nyanda za juu Wille Mponzi,alisema msaada huo ni kutokana na thamani kubwa wanayopewa na wananchi kwa kurejesha sehemu ya faida inayopatika.
“Kwa miaka mingi NMB imekuwa ikisadia miradi ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita zaidi katika miradi ya elimu kwa kutoa madawati,bati na vifaa vya kuezeka na kwenye sekta ya afya kwa kutoa vitanda,magodoro na vifaa tiba sambamba na majanga mbalimbali yanayoipata nchi.Msaada wa bati hizi zitakwenda kuboresha miundombinu na kuinua taaluma”alisema Mponzi.
Aidha Mponzi alisema benki hiyo imezifikia wilaya zote nchini kwa asilimia 100 na itaendelea kushirikiana na wadau wake kwa kuunga mkono katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo katika jamii.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada wa bati hizo na kisha kuzikadhi kwa uongozi wa shule waziri wa utamaduni sanaa na michezo nchini balozi Dk Pindi Chana,alisema benki ya NMB imekuwa mdau mkubwa wa serikali inasaidia kutekeleza miradi mingi katika jamii na kwamba wataendelea kuipa ushirikiano uliyotukuka katika utekelezaji wa majukumu yake.
Dr Pindi Chana alisema msaada wa bati 200 unakwenda kusaidia katika utekelezaji wa mradi wa bweni litakalotumika na wanafunzi na kisha kuwataka wanafunzi kuongeza bidii katika masomo kwasababu urithi pekee mzuri kwa watoto ni elimu.
“Nichukue nafasi hii kukabidhi mabati haya katika sekondari yetu ya Iwawa na tuendelee kumuombea Rais kwa sababu serikali inaendelea kutoa elimu bure kuanzia awali hadi sekondari na unapofika chuo kikuuu kuna bodi ya mikopo inawasubiri hivyo kazaneni”alisema Dr Pindi
Mbunge wa Makete Festo Sanga ameishukuru benki ya NMB kwa kulitatua tatizo katika shule ya sekondari Iwawa,hivyo serikali inaendelea na uboreshaji wa miundombinu kwani hadi sasa kata zisizo na shule ya sekondari ni Kigala na Buhongwa ambazo nazo itakapofika mwaka 2025 zitakuwa zimejengwa.
Awali akitoa taarifa ya shule hiyo,kaimu mkuu wa shule ya sekondari Iwawa Stanford Mwandelile alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa maktaba,upungufu wa walimu,madarasa pamoja na kukosekana kwa eneo la ujenzi kujenga miundombinu mingine yakiwemo mabweni na madarasa kwa sababu eneo la shule limejaa.
“Nitumie fursa hii kuwashukuru sana benki NMB kwa msaada wa bati hizi,zitakwenda kutumika katika jengo la bweni la wanafunzi wa kiume 600 kati ya 1047 wanalala bwenini kwa hiyo msaada huu utasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaokaa bwenini pamoja na kuinua kiwango cha taaluma kwa sababu nusu ya wanafunzi wanatoka majumbani”alisema Mwendelile.
Mmoja wa wanafunzi kidato cha sita shule ya sekondari Iwawa Mwidini Msingili,aliishukuru benki ya NMB kwa kuwapa msaada wa bati hizo kwa sababu zinakwenda kukamilisha ujenzi wa bweni ambalo litasaidia wanafunzi wengine kulala shuleni pamoja kupata muda mwingi wa kujisomea badala ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu.