…………………..
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuongeza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma atakayeshughulikia Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kukabiliana na changamoto za Ardhi jijini hapo.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula alipokuwa akiongea na wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wenye changamoto za kupewa ‘control number’ na madai ya hatimiliki yaliyochukua muda mrefu katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Dkt. Mabula alisema “kutokana na changamoto ya migogoro ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, tunakwenda kuongeza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma atakayeshughulikia Halmashauri ya Jiji la Dodoma pekee ili kumpunguzia mzigo wa Halmashauri nyingine za Mkoa wa Dodoma”.
Akiongelea maelekezo yake kwa wataalam wa Ardhi, alisema kuwa aliwaelekeza kupanga ratiba ya siku mbili kwa wiki siku ya Jumanne na Ijumaa kutoka ofisini kwenda katika maeneo ya watu badala ya wananchi kuwafuata ofisini.
“Leo nimekuja kusikiliza wananchi ambao wamekalimisha taratibu na malipo ya halmashauri lakini wanahitaji ‘control number’ kwa ajili ya malipo ya wizara…Pili wananchi ambao walishakamilisha taratibu zote lakini hatimiliki zao hawajapatiwa” alisema Dkt. Mabula.
Akiongelea migogoro iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, waziri aliitaja kuwa ni migogoro inayotokana na fidia.
“Wananchi maeneo yao yalichukuliwa kwa ajili ya maendeleo ya Dodoma tunayoyaona hapa na hawajalipwa fidia zao. Changamoto nyingine ni upimaji shirikishi wa mgawanyo wa asilimia 70 kwa 30. Upimaji huu haukwenda katika utaratibu ule tuliokuwa tunautegemea kama mkoa na halmashauri nyingine zilivyofanya.
Nyingine ni ‘double allocation’. Viwanja vilivyokuwa vimemilikishwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na wataalam wetu wa Halmashauri wakavimilikisha tena watu wengine. Matokeo yake kukawa na migogoro” alisema Dkt. Mabula.