NA
K-VIS BLOG, BUTIAMA
MFUKO
wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetoa msaada wa vifaa tiba
kwa vituo sita vya afya ikiwa ni kuunga mkono juhudi kubwa wanazofanya watumishi
wa umma katika kuwahudumia wananchi kwenye maeneo tofauti ikiwemo eneo la utoaji
huduma za afya.
Vituo
vilivyonufaika na msaada huo ni pamoja na kituo cha Afya Kirumi kilichoko
Wilaya ya Butiama Mkoani Mara ambacho kimekabidhiwa Ijumaa, Juni 30, 2023
na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA. Hosea Kashimba.
Akizungumza
kwenye hafla fupi ya kukabidhi vifaa hivyo, CPA. Kashimba alisema vituo vingine
vitano vikiwemo Mkunguni na Dimbani vilivyoko Kizimkazi, Zanzibar, Ikombe, Mtwara, Mji,
Lindi na Ilembo Mkoani Katavi, vilikabidhiwa vifaa kama hivyo wakati wa Wiki ya Utumishi wa Umma iliyofikia kilele chake Juni 23, 2023.
“Hapa
tuko mahala pake, nyote ni watumishi wa Umma mko hapa kuihudumia jamii ya wana
Kirumi tunaamini vifaa hivi tulivyokabidhi vitasaidia kuimarisha utoaji wa huduma
bora kwa wagonjwa wetu.” Alisema CPA. Kashimba, ambaye alifuatana na Meneja wa
Kanda ya Ziwa, Bw. Rajab Kinande, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wananchama, Bw.
James Mlowe na Meneja wa Mkoa wa Mara, Bi. Nyaswi Elias.
CPA Kashimba aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wake mahiri Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya afya nchini.
“Tunashuhudia maendeleo makubwa ya ujenzi wa miundombinu ya afya kila pembe nchini, ni wajibu wetu kama taasisi ya umma kuunga mkono mafanikio haya makubwa ya serikali.” Alifafanua Mkurugenzi huyo Mkuu wa PSSSF.
Akifafanua
zaidi alisema, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) ilitoa maelekezo kwa
taasisi za umma kuangalia namna bora ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma
kwa kuwatembelea watumishi wa umma walio pembezoni mwa nchi ili kujua changamoto
wanazokabiliana nazo katika kuwahudumia wananchi.
“Kubwa
ni kuwasisitizia watumishi kuhusu uwajibikaji mahali pa kazi na eneo ambalo
tulilichagua ni eneo la afya na hii ni kwa kutambua huduma za afya ni moja ya
mahitaji muhimu ya kila binadamu, kuimarisha utoaji huduma za afya ni kujenga
jamii iliyo na afya bora na hivyo kupelekea kulinda nguvu kazi na hatimaye
kuchangia uzalishaji na kuleta maendeleo ya taifa.” Alifafanua.
Kwa
upande wake, Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Mara, Bw. Msalika Makungu aliishukuru
PSSSF kwa kuwaunga mkono kwa kutoa vifaa hivyo.
“Tunaamini
kwa msaada wenu mliotoa sio tu kwamba mnawatia nguvu watumishi tu bali pia mnawaunga mkono wananchi ambao kwa nguvu zao ndio waliojenga kituo hiki cha afya.” Alifafanua Bw.
Msalika.
Alitoa
wito kwa viongozi na wananchi kuvitunza na kuwa walinzi wa vifaa tiba
walivyopokea.
“Hivi
karibuni katika baadhi ya maeneo hapa nchini kumetokea wizi wa vifaa tiba
kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya, na vifaa hivyo vinapoibiwa na
watu wasio waaminifu wasiojali matokeo ya vitendo vyao kunakuwa na changamoto
kubwa ya utoaji wa huduma.” Alisema na kuongeza….tuhakikishe yaliyotokea
kwingine yasitokee hapa Kirumi, na kwa kufanya hivyo tunawapa nguvu na moyo
hawa wanaotusaidia kwasababu wangependa kuona wananchi wanafaidika katika
utoaji wa huduma.
Aidha
Bw. Msalika aliwaomba wananchi kuwa walinzi wakuu kwani wahalifu hawawezi
kufika kijijini bila ya kuwa na wenyeji.
Picha ya pamoja
Mkurugenzi
wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi (wapili kushoto) na watumishi wa PSSSF
Ofisi ya Zanzibar, wakikabidhi vifaa kwenye Kituo cha Afya Mkunguni, Kizimkazi,
Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.