Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akiwa katika kikao cha wizara kwa ajili ya kuweka mikakati ya kutekeleza vipaumbele katika mwaka wa fedha ujao. Kikao kilichofanyika jijini Dodoma jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa kikao cha wizara kuweka mikakati ya kutekeleza vipaumbele katika mwaka wa fedha ujao. Kikao kilichofanyika jijini Dodoma jana.
…………………………..
Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema wizara yaje imeweka vipaumbele 12 katika mwaka ujao wa fedha 2023/2024 unaoanza Julai mosi mwaka huu lengo kubwa likiwa kuondoa changamoto za sekta ya ardhi na kutilia mkazo ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula katika kipindi cha mwaka huo wa fedha wa 2023/2024, Wizara ya Ardhi imejipanga kuhakikisha mikakati yake inaenda vizuri hususan kuondoa kero na malalamiko ya wananchi kwani dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nchi inakuwa kiuchumi na watu wake wanafaidika na mali waliyokuwa nayo ambayo ni ardhi.
Dkt Mabula alisema hayo jana tarehe 28 Juni 2023 ikiwa ni muda mfupi baada ya kikao cha uongozi wa wizara kwa ajili ya kuweka mikakati ya kutekeleza vipaumbele vya Wizara ya Ardhi baada ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti 2023/2024 ambapo kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi kabla ya viongozi kuanza kusambaa maeneo mbalimbali wameona wakutane na kuweka mikakati ya namna bora ya kufanyia kazi wanayotarajia kuyafanya katika mwaka wa fedha ujao.
‘’Kama wizara tumejipanga na tunatembelea maelekezo ya Mhe. Rais ambaye amaeonesha njia na tunafuata nyayo zake kuhakikisha changamoto, dhulma, migogoro, malalamiko hayana nafasi katika kipindi hiki na tutahakikisha watendaji wa sekta ya ardhi wanajipanga sawasawa katika kutenda kazi hiyo’’ alisema Dkt Mabula
Katika kutekeleza viaumbele hivyo, Waziri Dkt Mabula alisema moja ya mambo wanayokwenda kuyawekea mkazo ni suala la migogoro ya ardhi ambapo wizara yake kwa kushirikiana na mamlaka za upangaji inakwenda kuweka mikakati ya kumaliza migogoro na ikilenga zaidi mkoa wa Dodoma.
‘’Mkoa wa Dodoma tumeulenga zaidi kutokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi ambapo kama wizara tumeona mkoa huu sasa uwe na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wawili ambapo mmoja atashughulika na Jiji huku mwingine akishughulika na wilaya zilizopo pembezoni’’. Alisema Dkt Mabula
Akielezea zaidi vipaumbele hivyo, Dkt Mabula alisema, suala la makusanyo ardhi nalo wataenda kulitilia mkazo hasa ikizingatiwa Rais Samia ameshusha gharama za umulikishaji ardhi na wizara yake inakwenda kuwatangazia wananchi ushushwaji wa gharama hizo.
‘’Rais Mhe. Dkt Samia Saluhu Hassan ameridhia kushusha gaharama za umilikishaji ardhi na kwa sasa kuna takriban viwanja milioni moja na laki tano vimekamilika na ramani zake zimeidhishwa lakini wamiliki wake wameshindwa kuchukua, wizara tunakwenda kulisemea hilo’’ alisema Dkt Mabula.
Aidha, Sera na Sheria za Ardhi ni jambo linalopewa kipaumbele hasa ikizingatiwa tayari serikali imeleta nafuu wa gharama katika suala la uhamisho wa milki kutoka asilimia 10 hadi 3 sambamba kuondoa ile kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa ununuzi wa nyumba za gharama nafuu.
Kuhusu Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Dkt Mabula aliweka wazi kuwa vijiji vingi vimepimwa na kati ya vijiji 12,000, vijiji 10,000 vimepimwa na vina vyeti lakini changomoto ni mipango ya matumizi ya ardhi kutovifikia baadhi ya vijiji na kusisitiza kuwa, mamlaka za upangaji ambazo ni halmashauri zinatakiwa kuongeza kasi katika suala hilo kwa kushirikiana na Tume.
Waziri Dkt Mabula alizungumzia pia mradi wa Kupanga, kupima na kumikilisha ardhi (KKK) ambapo alisema, changamoto kubwa ya mradi huo ni kutorejeshwa mikopo kwa wakati na kueleza kuwa wizara yake inaangalia namna ya kuhakikisha fedha zinarejeshwa kwa wakati ufuatiliaji ukifanyika kuona kiasi kilichotumika lengo kuongeza kasi ya umilikishaji.
Vile vile, alielezea suala la Mifumo ya Tehama ambapo alibainisha kuwa, hilo ni moja ya jambo litakalotiliwa mkazo ambapo alisema kupitia mfumo kila mmiliki anaenda kusomeka na kueleza kuwa hiyo itaisaidia kutambua wamiliki sambamba na kusaidia katika ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
Akigeukia suala la Uendelezaji Milki, Dkt Mabula alisema, sekta hiyo bado haijaendelezwa kwa kiasi kikubwa na wizara yake itatupia jicho zaidi eneo hilo huku ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa kutumia teknolojia mpya ukipewa kipaumbele.
Aidha, Waziri Dkt Mabula amesema wizara yake pia inaangalia suala la uendelezaji maeneo yaliyochakaa sambamba kufungua wigo mpana kwa wandelezaji Milki lengo likiwa kuondokana na maeneo yaliyochakaa huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano pale mpango huo utakapoanza kwa kuwa wao ndiyo watakaonufaika.
Vipaumbele vingine kwa mujibu wa Waziri Dkt Mabula ni utoaji elimu kwa umma, masuala ya uwekezaji, uimarishaji mipaka ya kimataifa pamoja na fursa ya wananchi kutumia Kituo cha Mawasiliano kwa Wateja kitakachowawezesha kupatiwa huduma bila kufika ofisi za ardhi.