Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula anatarajia kukutana na Wananchi wa Dodoma Ikiwa ni hatua mahususi ya Kushughulikia Changamoto ya Mkwamo wa Upatikanaji Hatimiliki za Ardhi ndani ya Jiji hilo.
Hatua ya Dkt Mabula inakuja baada ya Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo kupitia ziara yake ya Siku 8 mkoani Dodoma kubaini uwepo wa migogoro ya Ardhi, huku akionesha kutoridhishwa na namna inavyoshughulikiwa.
Kwa Mujibu wa Taarifa kwa Umma iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeeleza kuwa Kikao cha Dkt Mabula na Wakazi wa Jiji la Dodoma kitafanyika Juni 30, 2023.
Pamoja na Mambo mengine kikao hicho kimelenga kutatua Changamoto ya Wananchi kushindwa kupata Namba Kwa Ajili ya Kufanya Malipo ‘Control Number’ pamoja na Mkwamo wa Wananchi kupata Hatimiliki ingawa wamekamilisha taratibu zote za Kupatiwa hati.
Aidha Taarifa hiyo ya Wizara ya Ardhi imeongeza kuwa mkutano huo wa Siku moja umepangwa Kufanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji Dodoma Mjini Mkabala na Maktaba ya Mkoa Kuanzia Saa tatu kamili asubuhi.