…………………..
CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA)kimeipongeza Serikali kwa kuruhusu huduma za usafiri wa Mabasi kutolewa kwa Saa 24 kwa kusisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza uchumi wa nchi kama ilivyo kwa mataifa mengine.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mweka Hazina wa Taboa ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Usalama Barabarani la Taifa Issa Nkya muda mfupi baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuahirisha shughuli za Bunge Jijini Dodoma jana ambapo pamoja na mambo mengine alisema Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kujilidhisha na uwepo wa miundombinu mizuri ya barabara, usalama wa kutosha pamoja na utayari wa watoa huduma.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukisikia kilio chetu cha muda mrefu kwa kuturuhusu kutoa huduma za usafiri kwa Saa 24, ukweli kama nchi tulichelewa kutoa huduma hiyo kutokana na kuwa na manufaa mengi hasa katika eneo zima la kukuza uchumi wetu” alisema Nkya
Alisema wao kama wasafirishaji wanaona kuanza kutolewa kwa huduma hiyo za usafiri kwa saa 24 kwa kiasi kikubwa kutasaidia kuchagiza ukuaji wa maendeleo ya nchi katika sekta zote kutokana na ukweli kuwa sekta a usafirishaji ni kiungo kikuu cha kufanikisha maendeleo ya sekta zingine hapa nchini na Duniani kwa ujumla.
Akitolea mfano katika hilo, alisema kwa wiki chache tangu huduma za mabasi zianze kutolewa kwa ratiba inayoanzia saa 9 usiku, kumesaidia wasaifiri wanaoenda mikoa mbalimbali nchini na hata nje ya nchi kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kuwahi kurejea katika maeneo yao ndani ya muda na kusisitiza kuwa kuanza kutolewa huduma hizo kwa muda wote wa Saa 24 kutaongeza tija zaidi.
“Aidha pamoja na Shukrani zetu kwa Rais Samia sisi kama wasafirishaji pia tunapenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Spika wa Bunge Dk Tulia Akson kwa kulisimamia suala hadi leo hii tulipofika hapa, ukweli tunawashukuru sana viongozi wetu hawa kwa kuzingatia maslahi ya taifa” aliongeza Nkya.
Kwa upande wake Msemaji wa Taboa Hashemu Mwalongo pamoja na pongezi hizo ameiomba Mamlaka ya Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu nchini (LATRA) kutoa ratiba za mabasi hayo ili mabasi yaweze kusafiri nyakati tofauti ndani ya Saa 24 hatua aliyosisitiza kuwa kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza tabia ya madereva kukimbizana.
Alisema wao kama wamiliki wa mabasi wanaamini kama Latra itatoa ratiba ya Saa 24, pia itawapa mwanya mpana abiria kuchagua muda wa kusafiri ili kufika maeneo wanayoyataka katika muda wanaoona unawafaa jambo ambalo pia kwa namna moja au nyingine itaondoa usumbufu kwao wa namna tofauti.
Aidha alisema Taboa imejipanga kikamilifu kuhakikisha inaendelee kutoa huduma zake kwa kiwango cha kikubwa huku ikiwataka madereva kuzingatia sheria zote za Barabarani ili kulinda usalama wa abiria pamoja na magari kwa ujumla akidai kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kulinda ustawi wa Taifa na jamii kwa ujumla.
Ends