……………
Na Mwandishi wetu, Mirerani
TAASISI ya Ahasante Foundation Tanzania katika kusherehekea sikukuku ya Eid Al adha, imechinja ng’ombe 600, kondoo na mbuzi 2,000 na kugawa kwa wajane, wagane, yatima na taasisi mbalimbali za Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Mwenyekiti wa taasisi ya Ahasante Foundation Tanzania, Katada Kimaro amesema mifugo hiyo imechinjwa kwa lengo la kutolewa sadaka kwa wahitaji.
Kimaro amesema taasisi hiyo pia imechinga mifugo kwenye maeneo tofauti ikiwemo kata ya Makiba ng’ombe 50 na mbuzi 200 na Mirongoine ng’ombe 150 wilayani Arumeru mkoani Arusha na mkoa wa Singida.
Amesema taasisi hiyo imefanikisha tukio hilo kwa kushirikiana na taasisi ya Paylas Kurbanini Kurban 2023 ya kutoka nchi ya Uturuki.
“Walengwa hasa ni wale wahitaji ikiwemo wajane, wagane, yatima, wagongwa na wahitaji mbalimbali ikiwemo taasisi za binafsi na za serikali ikiwemo kituo cha afya Mirerani,” amesema Kimaro.
Mmoja kati ya wahitaji waliopata msaada huo Mariam Hamis amezishukuru taasisi hizo kwa kuwapatia kitoweo kwenye sikukuu hiyo.
“Hii ni sikukuu ya Eid Al adha ya kuchinja na mimi na wanangu tunapata kitoweo na kufurahia sherehe ya idi kama watu wengine wanavyofurahi,” amesema.
Kasim Omary ameishukuru taasisi hiyo kwa kugawa kitoweo kwa wahitaji mbalimbali hasa wanawake wajane, wagane, yatima na taasisi mbalimbali.
“Mwaka jana 2022 taasisi hii ilifanya hivi hivi kwa kusaidia jamii katika sikukuu ya idi tunawashukuru mno kwa kurudia tena mwaka huu
,” amesema.
MWISHO