Kenta lililokuwa limebeba mitungi ya gesi ikitokea Jijini Mwanza iliyogongana na gari ya abiria iliyokuwa ikitokea Misasi Wilayani Misungwi.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Gidioni Msuya
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Watu zaidi ya 40 wamenusurika kifo katika ajali iliyohusisha basi dogo la abiria aina ya Tata lenye namba za usajili T 127 DHH iliyokuwa ikitokea Misasi wilayani Misungwi kugongana na gari la mizigo aina ya kenta yenye namba za usajili T 482 DQS iliyokuwa imebeba mitungi ya gesi ikitokea Jijini Mwanza.
Wakizungumza na Fullshangwe Blog baadhi ya abiria walionusurika katika ajali hiyo wameeleza namna ilivyotokea huku wakimshukuru dereva wa gari la abiria kwa kujitahidi kuokoa maisha yao kutokana na gari aina ya Kenta kukatiza barabara kwa kushtukiza.
Kwa upande wake Dereva wa gari lililokuwa limebeba mitungi ya gesi Steven Mahodole, amesema ajali hiyo imetokea wakati akitoka kwenye barabara kuu kuingia barabara ya vumbi ndipo gari ya abiria ikawa imefika na kuigonga gari yake ubavuni na kisha kuanguka.
Katika ajali hiyo pia gari la abiria limegonga gari dogo lililokuwa limepaki lenye namba za usajili T457 DYK ambapo mmliki wa gari hilo David Cham, amesema kuwa hakukua na mtu ndani ya gari.
Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu Kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza Gidioni Msuya amekiri kutokea kwa tukio hilo majira ya saa 5 asubuhi katika eneo la Nyangomango wilayani Misungwi ambapo amesema hakuna majeruhi wala vifo na kwamba jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo.