Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Bi.Rehema Madenge, amewataka wadau wa afya mkoani humo, kushirikiana kwa karibu na Bohari ya Dawa (MSD) ili kuboresha huduma na kutatua changamoto mbalimbali zinazoukabili mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya mkoani humo.
Bi. Madenge ametoa rai hiyo hapo jana, wakati akifungua kikao kazi baina ya Bohari ya Dawa (MSD), Kanda ya Dar es Salaam na wadau wake wa afya mkoani humo, waliokutana kwa lengo la kujadili namna bora ya kuboresha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, huduma na mahusiano baina ya pande hizo mbili.
Alisisitiza kwamba kikao kazi hicho cha wadau ni muhimu kwa kuwa kinajumuisha watendaji wa sekta ya afya kutoka serikali za mitaa hadi mkoa, hivyo kuipongeza MSD kwa hatua hiyo kwani itasaidia kuboresha hali ya utoaji wa huduma sambamba na utendaji kazi.
“Wito wangu watendaji wa vituo vya afya ni lazima kuzingatia takwimu sahihi za maoteo na mahitaji yao na kupeleka kwa wakati MSD, kuzingatia ukusanyaji wa mapato na kujaza fomu za bima ya afya kwa usahihi kuwezesha fedha kupatikana, ili wenzetu wa MSD waweze kutuhudumia kwa wakati, na wananchi waweze kunufaika,”alisema.
Akizungumza katika kikao kazi hicho Meneja wa MSD- Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Betia Kaema, amesema lengo la kikao kazi hicho ni kuboresha huduma za upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati katika vituo 960 na wilaya 23 wanazo zihudumia, katika Kanda hiyo.
Alisema, katika kikao hicho wamejadili kwa kina namna wanavyoweza kuboresha huduma za upatikanaji dawa na vifaa tiba katika maeneo yote wanayoyahudumia na kuweza kufikia adhima ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya huduma bora za afya kwa jamii.
Alisema kikao hicho kimewasaidia kubadilishana uzoefu, kujadili na kutatua kwa pamoja changamoto zilizopo kati ya watendaji wa MSD na watendaji wa afya mkoa humo, wakiwemo madaktari, wafamasia na wataalam wa maabara wa mkoa wa Dae es Salaam na kutoka na maadhimio ya pamoja.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Sallam Dk. Rashid Mfaume, alisema wanamshukuru Rais Dk.Samia kwa uwezeshaji mkubwa na utendaji wa MSD ambapo wanufaika wake ni wananchi, huku akiitaka MSD kuendelea kuboresha maeneo machache yaliyobaki, hasa manunuzi maalum (Special Procurement) na bidhaa za maabara
Alisema, kwa sasa vituo vya kutolea huduma mkoani humo vinapoagiza bidhaa vinapata kwa wakati hali inayosababisha uwepo wa dawa na vifaa tiba vya kutosha hususani zile dawa muhimu, hali iliyopunguza kero na malalamiko ya wananchi