Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
…….
Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Takwimu zinaeleza kuwa miji inakadiriwa kuzalisha asilimia 80 ya ukuaji wote wa uchumi.
Hivyo hakuna shaka kuwa Mji wa Serikali nchini Tanzania ambao upo katika Kata ya Ihumwa kilomita 17 kutoka katikati ya mji wa Dodoma wenye ukubwa wa ekari 1,542.88 uliogawanyika katika maeneo tofauti ya Wizara za Serikali, Ofisi za Mabalozi, Nyumba za Serikali, Huduma za Jamii, Maeneo ya Biashara, Bunge, Mahakama, Maegesho ya Magari na Eneo la Majitaka inaelezwa kuwa hadi kukamilika kwake unakadiriwa kugharimu shilingi za Kitanzania trilioni 10,709,176,758,503 utasaidia kuchochea uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Dodoma kwa kuibua fursa mpya za ajira ikiwa ni pamoja na kubadilisha mandhari ya mkoa huo.
Akizungumza leo Juni 28, 2023 bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa hoja ya kuahirisha Bunge, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alisema kuwa katika kukamilisha azma ya kuhamia Dodoma, Serikali inaendelea na ujenzi wa majengo 29 ya ghorofa katika Mji wa Serikali katika eneo la Mtumba ambapo kati ya majengo hayo 26 ni ya Ofisi za Wizara na matatu ya Taasisi.
Alifafanua kuwa hadi kufikia Juni 16, 2023 jumla ya shilingi bilioni 321 zimetolea kwa wakandarasi na washauri elekezi kwa ajili ya ukamilishaji wa majengi hayo.
Vilevile, ujenzi wa majengo hayo unaendelea sambamba na ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji safi, maji taka, umeme, gesi, mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, usalama, zimamoto na uokoaji na taratibu za programu za upandaji wa miti.
“Nitumie fursa hii katika kuzisisitiza Wizara na Taasisi ziharakishe ujenzi wa majengo yake ili kuanzia Januari 2024 majengo hayo mapya yaanze kutumika”, alibainisha Mhe. Waziri Mkuu.
Sambamba na ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wizara katika eneo la Mtumba, Mhe. Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa Uwanja wa Mashujaa ambapo kutakuwa na Mnara wa Mashujaa na bustani ya mapumziko katika eneo la Mji huo wa Serikali.
“Mradi huo unatekelezwa kwa awamu ambapo katika awamu ya kwanza unahusisha ujenzi wa uwanja wa gwaride. Mhe. Spika, ujenzi wa uwanja wa gwaride unatarajiwa kukamilika mapema ili kuwezesha Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa tarehe 25 Julai 2023 kufanyika katika uwanja huo”, Alieleza Mhe. Waziri Mkuu.