Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde akikagua moja ya miundombinu ya elimu inayojengwa katika Halmashuri ya Wilaya ya Uyui akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde akihimiza uwajibikaji kwa Menejimenti ya Halmashauri ya Mji wa Nzega katika kikao kazi chake cha kuhimiza uwajibikaji na kufanya tathmini ya ziara yake ya kukagua ujenzi wa miradi ya miundombinu ya elimu kwenye Halmashauri hiyo.
Baadhi ya watendaji wanaounda Menejimenti ya Halmashauri ya Mji wa Nzega wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde wakati wa kikao kazi chake cha kuhimiza uwajibikaji na kufanya tathmini ya ziara ya kukagua ujenzi wa miradi ya miundombinu ya elimu kwenye Halmashauri hiyo
………..
Na: James Mwanamyoto – OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde amewataka Maafisa Elimu na Maafisa Utumishi pamoja na watendaji wengine kuwahudumia vizuri walimu pindi wanapowasilisha changamoto zao ili zifanyiwe kazi.
Dkt. Msonde amesisitiza utoaji wa huduma bora kwa walimu nchini, wakati wa vikao kazi vyake na Menejimenti za Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Igunga na Nzega Mji ambavyo vililenga kuhimiza uwajibikaji na kufanya tathmini ya ziara yake ya kukagua ujenzi wa miradi ya miundombinu ya elimu katika Halmashauri hizo.
Dkt. Msonde amesema, walimu wanalalamika kujibiwa vibaya pindi wanapowasilisha changamoto zao kwa watendaji, na kuongeza kuwa Maafisa Elimu na Maafisa Utumishi ndio wanaolalamikiwa sana kwa kutoa kauli mbaya dhidi ya walimu ambao ndio wamepewa jukumu kubwa la kulea watoto na kuwapatia ujuzi.
“Walimu wanalalamika na kuwasilisha ushaidi wa sauti zilizorekodiwa za maafisa wote waliowajibu vibaya, ukisikiliza namna Afisa Utumishi au Afisa Elimu alivyomjibu mwalimu inaumiza sana na unaweze kutokwa na machozi hivyo wanapaswa kubadilika,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Dkt. Msonde amesema, maafisa hao wanapaswa kufahamu kuwa Mtumishi wa Umma anapaswa kutoa huduma nzuri kwa watumishi wengine na wananchi wanaofuata huduma katika maeneo yao ya kazi.
Ameongeza kuwa, mwalimu au mtumishi yeyote akiwasilisha hoja hata kama haina mashiko asijibiwe vibaya, akitoa mfano wake mwenyewe na wa Mhe. Waziri kuwa wanapokea malalamiko ya walimu 200 hadi 300 kwa siku lakini hawatoi kauli mbaya kwa walimu hao.