Baadhi ya wafanyakazi serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wa taasisi mbalimbali ikiwemo Shirika la Umeme Zanzibar pamoja na Wakala wa Barabara wakiwa darasani Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wakipata mafunzo ya makubaliano ya kibiashara pamoja na usimamizi wa mikataba tarehe 27/6/2023.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Dkt. Mwaige Mwasimba ambaye ni mkufunzi wa kozi mbalimbali ikiwemo mafunzo ya makubaliano ya kibiashara pamoja na usimamizi wa mikataba akifundisha wanafunzi kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi tarehe 27/6/2023.
Baadhi ya wafanyakazi Serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wakiwa darasani Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wakipata mafunzo ya makubaliano ya kibiashara pamoja na usimamizi wa mikataba.
Mkufunzi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Mwaige Mwasimba (kulia) akitoa maelekezo kwa mshiriki wa mafunzo ya makubaliano ya kibiashara pamoja na usimamzi wa mikatata.
Wanafunzi wa mafunzo ya muda mfupi kozi ya makubaliano ya kibiashara pamoja na usimamizi wa mikataba wakiwa katika picha ya pamoja na Mkufunzi Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Dkt. Mwaige Mwasimba.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wametoa mafunzo ya makubaliano ya kibiashara pamoja na usimamizi wa mikataba kwa wafanyakazi kutoka Serikali ya Tanzania Bara na Viziwani Zanzibar jambo ambalo litawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi.
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Dkt. Mwaige Mwasimba, amesema kuwa lengo ni kuwajengea uwezo taasisi za umma, sekta binafsi pamoja na mtu moja moja ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uweledi.
Dkt. Mwasimba ni mkufunzi katika mafunzo hayo, amesema kuwa Chuo Kikuu Mzumbe wamekuwa mstali wa mbele katika kuhakikisha watanzania wanakuwa na uwezo mkubwa wa kusimamia mikataba ili kuendana na thamani ya halisi ya fedha katika miradi inayotekelezwa.
Dkt. Mwasimba amesema kuna mafunzo ya muda mfupi ya siku tano yenye lengo ya kuhakikisha wafanyakazi wanajua na kutekeleza kadri ya mkataba unavyoelekeza.
“Pia kuna mafunzo yanaendelea hapa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam ya mtandano katika manunuzi ya umma” amesema Dkt. Mwasimba.
Dkt. Mwasimba amebainisha kuwa Taifa la Tanzania bado kuna changamoto ya majadiliano ya kibiashara na usimamizi wa mikataba katika kazi nyingi ambazo zinafanyika.
“Tunawakaribisha washiriki wengine kutoka taasisi za umma, binafsi na mtu mmoja mmoja kuja kujifunza ili kuongeza ufanisi katika utendaji” Dkt. Mwasimba.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo, Afisa Manunuzi Shirika la Umeme Zanzibar Bi. Sharifa Shemazi, ameishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa kutoa mafunzo ambayo yanakwenda kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Mafunzo yametusaidia kuwa na uwelewa mzuri kuhusu makubaliano ya kibiashara na mikataba, tuendelee kujifunza, taasisi mbalimbali zitoe fursa kwa wafanyakazi kujiendeleza kimasomo” amesema Bi. Shemazi.
Mhandisi Mtambo, Wakala wa Barabara Zanzibar Bw. Amini Ally, amesema kuwa wamejifunza mambo mengine ikiwemo muundo wa mikataba na changamoto zinazoweza kujitokeza na namna ya kutatua katika utekelezaji.
Amesema kuwa mafunzo hayo ni rafiki kwao hasa katika kufanya makubaliano ya kibiashara na kuingia mikataba.
“Chuo Kikuu Mzumbe katika mafunzo ya muda mfupi wapo vizuri, naomba taasisi nyengine zinazohusika na manunuzi waje kupata mafunzo ili waweze kufanya vizuri katika utendaji” amesema Bw. Mhandisi Ally.