Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent L. Bashunga (Mb) ametembelea na kukagua utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa kimataifa wa Golf unaotekelezwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) eneo la Ihumwa, Jijini Dodoma.
Mradi huo, unajumuisha viwanja 18 vya mchezo wa Golf, Hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano na viwanja vya michezo mbalimbali, mabwawa ya kuogelea, bustani ya kufugia Wanyama (zoo), ambapo maandalizi ya viwanja tisa umekamilika.
Uwanja huo utakapokamilika utakuwa ni uwanja mkubwa na wa kisasa kuwahi kujengwa hapa nchini na kufuatiwa na Uwanja wa TPDF Lugalo Golf Club, ambao pia unamilikiwa na JWTZ na kuifanya JWTZ kuwa Taasisi pekee nchini iliyojenga viwanja vyake, kwani viwanja vilivyopo vimejengwa na wakoloni.
Mara baada ya kukagua, Waziri Bashungwa amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kutekeleza vyema dira na maono ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kulipa Jeshi fursa ya Kujenga Uwanja wa Golf mkubwa na wa kisasa pamoja na Hoteli yenye ya kisasa yenye hadhi ya nyota tano.
Aidha, Waziri Bashungwa amewapongeza Majenerali kwa kuasisi na kuanza kutekeleza Mradi huo kabambe ambao si tu kwamba utakuwa chanzo cha mapato, lakini pia, utasaidia kuitangaza nchi yetu nje ya nchi.
Kuhusu changamoto zinazokabili utekelezaji wa mradi huo, Waziri Bashungwa ameahidi kukutana na viongozi wenzake ngazi ya Wizara na mawaziri wengine hususan Wizara ya Maji na Ujenzi na Uchukuzi, kuona ni kwa namna gani wataweza kutatua changamoto zote, ili mradi huo uweze kukamilika kama ulivyokusudiwa.
Kulingana na eneo panapojengwa Uwanja huo (Dodoma) lenye ekari 573, Waziri Bashungwa ametoa rai kwa JWTZ kuwa eneo hilo limekaa kimkakati lakini ni dogo, hivyo basi, ni vyema ukaangalia uwezekano wa kuliongeza ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa wanaoishi kuzunguka eneo hilo.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati inayotekeleza Mradi huo, Brigedia Jenerali Hassan Mabena ambaye pia ni Mkuu wa Utawala wa JKT, amesema kuwa Mradi huo umepangwa kutekelezwa kwa Awamu tatu kwa kutumia vyanzo vya mapato ya ndani, awamu ya kwanza itakayogharimu jumla ya Shilingi milioni 253.6 kwa kujenga viwanja tisa, kujenga mkuza, kuchimba visima na uwekaji umeme.
Vile vile, Jenerali Mabena ametaja faida mbalimbali zitakazotokana na mradi huo, kuwa ni pamoja na kuwa sehemu salama ya kulaza wageni wa ndani na nje ya nchi, kujenga mfumo wa kupendana baina ya wanajeshi na raia, usalama kwa viongozi wa kitaifa na kijeshi, ajira kwa wananchi kwenye hoteli, viwanja vya michezo na Golf pamoja na kuwa chanzo kimojawapo cha mapato.