Profesa Musambayi Katumanga (wa pili kushoto) wa Chuo Kikuu cha nchini Kenya na mgeni rasmi katika Kongamano la 14 la Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha Umajumui wa kiafrica (Pan Africanism) akizinduwa rasmi kitabu cha Hakielimu cha ‘Kiswahili – Lugha ya Kufundishia Kikwazo cha Usawa katika Kujifunza na Upimaji Tanzania’. Kulia ni Mwenyekiti wa kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha umajimui wa Africa, Profesa Rwekaza Mukandala na meza kuu wakishuhudia. |
Na Joachim Mushi, Dar
TAASISI ya Hakielimu imezinduwa kitabu
kinachojenga hoja na kuchochea matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Tanzania
inaweza kutumika kama lugha ya kufundishia kwenye ngazi ya shule za sekondari
pamoja na vyuo vikuu.
Kitabu hicho kimezinduliwa jijini Dar es Salaam na Profesa
Musambayi Katumanga wa Chuo Kikuu cha nchini Kenya mgeni rasmi katika Kongamano la 14 la Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha Umajumui wa kiafrica (Pan
Africanism), Chuo Kikuu cha Dar as Salaam.
Akizungumzia kitabu hicho mara baada ya kuzinduliwa, Mhariri
wa Kitabu na Mshauri Mwelekezi wa Hakielimu, Dk. Wilberforce Meena allisema
kitabu hicho kinazungumzia jinsi ambavyo Tanzania kwa sasa inaweza kutumia
lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia, hasa katika ghazi ya Shule za
Sekondari na Elimu ya juu.
Alisema kuwa, kitabu hicho kilichopewa jina la ‘Kiswahili – Lugha
ya Kufundishia Kikwazo cha Usawa katika Kujifunza na Upimaji Tanzania’ kimejumuisha
makala anuai zilizoandaliwa na wataalam waliobobea katika lugha, ambao
wameelezea jinsi ambavyo Kiswahili kwa wakati huu kimefikia uwezo wa kutumika
kama lugha ya kufundishia katika shule na vyuo vyetu nchini Tanzania.
“…Tunafikiri kuwa kwa kuzinduwa kitabu hiki na haswa kwa wale
watakaopata muda wa kukisoma kitazidi kuwapanua, kuwaonesha jinsi ambavya sisi
kama nchi tunaweza kutumia Kiswahili katika elimu yetu…kumekuwa na mjadala kwa
muda mrefu juu ya matumizi ya Kiswahili na lugha ya kiingereza katika
kufundishia, lakini kitabu hiki kinajaribu kujibu maswali ya mjadala huu kwa
kiasi kikubwa sana” alisema Dk. Meena ambaye pia ni Mhariri wa kitabu hicho.
Akifafanua zaidi Dk. Meena alibainisha kuwa makala katika
kitabu hicho zinaonesha wazi kuwa mpaka sasa Tanzania imechelewa katika kufanya
maamuzi juu ya matumizi ya lugha ya Kiswahili kufundishia hasa ngazi ya
sekondari na vyuoni. “..kimsingi wakati umefika sasa wa kuanza kukitumia
Kiswahili kufundishia katika elimu yetu ya sekondari na elimu ya juu,” alisema.
“Kitabu hiki ni msaada mkubwa kuendelea kujenga hoja hasa kwa
watetezi wa lunga ya Kiswahili nchini kwenye mjadala unaoendelea juu ya
matumizi ya lugha ya Kiswahili kutumika kufundishia kwenye ngazi ya shule za sekondari
na vyuoni.
Aidha akijibu hoja ya kwamba huenda lugha hiyo ikashindwa
kujitosheleza kimsamihati alisema lugha hiyo inajitosheleza na ni jambo la
kawaida lugha kutohoa maneno kutoka lugha nyingine pale inapobidi.
Pamoja na hayo aliongeza kwamba Kiswahili kinajitosheleza na
kuungwa mkono, kwani hata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam taasisi ya Uchunguzi wa
Kiswahili (UDSM) hapo nyuma waliwahi kuandika vitabu vya Kiswahili kwa masomo
ya Sayansi kwa ajili ya matumizi ya shule za sekondari.
“Kiswahili kinajitosheleza katika kutumika kufundishia na bado
kuna fursa hata ya kuendelea kutohoa baadhi ya maneno kutoka katika lugha nyingine pale inapobidi,
kwani hata kiingereza kinachotumika kwa sasa yapo maneno mengi yametoholewa
kutuka katika lugha zingine,” alisisitiza mhariri huyo wa kitabu.