Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb), amekuwa Mgeni Rasmi akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika adhimisho la Misa Takatifu ya kumpokea Mhashamu Askofu Mkuu Mwandamizi Protase Rugambwa aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu, Papa Francis kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora.
Kupitia adhimisho hilo Nape amewasilisha salamu za Rais Samia za kumpongeza na Kumkaribisha Askofu huyo mpya kwa kusema kuwa.
“Kama Serikali tunamshukuru sana Baba Mtakatifu Francis kwa kututeulia Mchungaji mwema katika Jimbo letu la Tabora. Tunafahamu kuwa Mhashamu Baba Askofu Mkuu Mwandamizi amekuwa mtendaji katika kurugenzi mbalimbali chini ya Ofisi za Baba Mtakatifu huko Roma ikiwa ni pamoja na kuwa Katibu Mkuu wa Idara ya Uinjilishaji Ulimwenguni. Mhashamu Rugambwa ni tunda la Tanzania, Baraka kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa uongozi wake uliotukuka hadi kuwa kiongozi wa Kimataifa ambayo ni sifa kwa nchi yetu”.- amesema Nape.
Sambamba na hilo Nape amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Kiuchumi na Kijamii kwa ajili ya Maendeleo ya Watanzania, na kusimamia misingi ya utu kwa kutoingilia uhuru wa kuabudu kwa watu wote.
Pia Nape ametumia wakati huo kwa kutoa rai kwa viongozi wote wa dini nchini kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maadili kwa watu wote ambao ndio msingi wa ustawi wa Taifa.
Misa Takatifu imefanyika kwenye Kituo cha Hija cha Ifucha na kuhudhuriwa na Viongozi wengine mbalimbali wa Serikali, Viongozi wa Dini, Viongozi wa vyama vya siasa na Waumini wa wa Katoliki.