Wizara ya Maji imepongezwa kwa kukamilisha Programu ya Uwekezaji katika Sekta ya Maji (TanWIP) 2024-2030 hapa nchini, ambayo utekelezaji wake utakuwa na thamani ya Dola za Marekani Bilioni 15.02
Rais wa mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa pongezi hizo alipoongea na menejimenti ya taasisi za Sekta ya Maji jijini Dodoma, katika ukumbi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Mhe. Dkt. Kikwete amesema hatua iliyopigwa na Serikali ya Awamu ya Sita ni kubwa kwa sababu lengo la “kumtua mama ndoo ya maji kichwani” linakamilishwa ikiwamo kuhakikisha maji yanapatikana ndani ya mita 400 kutoka katika makazi, na sio wananchi kusafiri kwenda kutafuta huduma ya maji.
Ameongeza kuwa mapinduzi na mabadiliko makubwa yamefanyika katika kuihudumia jamii katika eneo la maji, ukilinganisha na historia ilivyokuwa zamani pamoja na juhudi za dhati zilizokuwa zikifanywa na viongozi wa ngazi tofauti tofauti katika kufanikisha utekelezaji wa miradi wa maji.
Mhe. Rais Dkt. Kikwete katika historia ya uongozi wake aliteuliwa kuwa Waziri wa 10 kuhudumu katika Sekta ya Maji tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiongea katika kikao hicho amesema Sekta ya Maji na kazi zake kwa ujumla imebebwa na watu wengi, na viongozi mbalimbali akiwemo Mhe. Kikwete, ambaye alifanya kazi kubwa ya kutukuka na hadi leo bado anatumika kujenga kizazi kipya katika kazi.
Mhe. Aweso amesisitiza wazee katika jamii wana mchango mkubwa katika maendeleo yanayotokea leo na mabadiliko mbalimbali katika utendaji kazi, hivyo ni vizuri watumike.
Akielezea program hiyo ya TanWIP Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba amesema imejikita katika maeneo makuu manne ambayo ni maji kwa uchumi endelevu, maji kwa ustawi wa jamii, masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na menejimenti ya rasilimali za maji.
Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taaisi inayojishughulisha na masuala ya maji, Global Water Partnership Southern Africa (GWPSA) na Mwenyekiti Mwenza Mbadala (Alternative Co-Chair) wa Programu ya Uwekezaji katika Maji barani Afrika, Continental Africa Water Investment Programme (AIP) High-Level Panel.