Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo akitembelea kiwanda cha Mbolea cha Intracom jijini Dodoma.
Na. Dennis Gondwe, NALA.
WAFANYAKAZI wa Kiwanda cha Mbolea cha Intracom wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu ili kujipatia maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa Kiwanda cha Mbolea cha Intracom kilichoko katika Kata ya Nala Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Kwa wafanyakazi hongereni kwa kazi. Mmepata fursa ya kufanya kazi, mfanye kazi kwa kujituma, uadilifu na uaminifu.
Mjitume kutafuta tija ambayo inatakiwa kwa pande zote, kwa muwekezaji na kwetu sisi wafanyakazi.
Huwa tunafikiri kinapoharibika, kinaharibika cha mwingine na sisi tunabaki salama.
Lakini kikiharibika sisi ndiyo wa kwanza kupata madhara. Mimi ndiyo wa kwanza kukaa nyumbani kisha mwekezaji ndo anafuata kutegemea na aina ya hasara. Tufanye kazi kwa moyo ili kulinda ajira zetu lakini tujitume zaidi ili waongeze mishahara. Tujiepushe na udokozi” alisema Chongolo.
Katibu Mkuu Chongolo aliitaka menejimenti ya kiwanda hicho kuwekeza kwenye utafiti.
“Niwaombe sana kuwekeza kwenye utafiti wa udongo wetu kwa kulinganisha na mbolea mnayozalisha ili tija tunayoanza kutangaza sasa iwe endelevu. Tija hiyo iwe ya muda wote kuliko baadae ije kuonekana na changamoto kwenye baadhi ya maeneo” alisema Chongolo.
Akiongelea changamoto ya Maji inayowakabili wakazi wa Kata ya Nala, alisema kuwa ufumbuzi utafutwe kupitia mpango wa Maji unaopelekwa katika kiwanda hicho.
“Mpango wa kupeleka Maji kiwandani lazima uende sambamba na kutoa huduma hiyo kwa kiwanda na wananchi pia. Tukipeleka Maji kwenye kiwanda pekee hata kama ni mimi ningelalamika.
Ndiyo ukweli na tukipeleka kwa wananchi na kiwandani hakuna Maji maana yake tija hatuwezi kuipata kwa wakati. Ni lazima twende kwa kuangalia pande zote.
Kwenye uwekezaji wa namna hii ni lazima wataalam wetu wawe wanajua kuweka usawa wa vitu hivi ili wananchi wasimchukie muwekezaji kwa sababu ya matatizo yetu ya kuwanyima huduma. Katibu Mkuu wa CCM taifa alifanya ziara katika Wilaya ya Dodoma alitembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani hapo.MWISHO