Na. Brigitha Kimario – Morogoro
Mradi wa Serikali chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) umeandaa ziara ya mafunzo kwa wananchi kutoka vijiji 15 vilivyopo Jirani na Hifadhi za kipaumbele cha mradi huo ambazo ni Ruaha, Udzungwa, Mikumi na Nyerere. Wananchi hao wapatao 60 wakiambatana na wataalamu wa Halmashauri za wilaya na Hifadhi; watatembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti, Tarangire na Manyara ili kujifunza kwa pamoja shughuli za Uhifadhi, na Utalii pamoja na jinsi jamii ziishizo pembezoni mwa Hifadhi hizo zinavyonufaika na fursa zitokanazo na uhifadhi na utalii.
Sambamba na ziara hiyo kikao cha kuelimisha wajumbe wa ziara kilifanyika ili kujenga uelewa wa pamoja na kubaini maeneo muhimu ya kujifunza kupitia ziara hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mratibu wa Mradi REGROW TANAPA wakati wa ufunguzi wa kikao hicho mjini, Morogoro Dkt. Halima Kiwango ambaye ni Afisa usalama wa mazingira na jamii katika mradi kwa upande wa TANAPA; amewaeleza wananchi hao kuwa kikao hicho na ziara ya mafunzo iwe kichocheo cha kubadili mtazamo na kuongeza uelewa kuhusu Uhifadhi na Utalii na kuwaasa kuchangamkia fursa zilizopo katika mnyororo wa sekta ya utalii na uhifadhi.
” Katika ziara mtajifunza Uhifadhi na Utalii na manufaa yake kijamii, kiuchumi na kimazingira. Mtaweza kubadilishana uzoefu na vikundi mtakavyotembelea, kujua mbinu mpya za kutatua changamoto mnazokutana nazo katika vikundi vyenu hivyo ni vema mkayachukua yaliyo mazuri ili kuboresha utendaji katika vikundi vyenyu.” Alisema Dkt. Kiwango
Naye, Msimamizi kipengele cha pili cha Mradi, Hobokela Mwamjengwa alibainisha TANAPA kupitia Mradi wa REGROW wamefungua fursa katika vijiji 61 kwa kutoa elimu ya Uhifadhi na Utalii ambayo imewezesha wananchi kujiunga katika vikundi na kunufaika.
“Tunategemea muwe mabalozi wazuri kwa wenzenu haswa katika vikundi mlivyojiunga vya ujasiriamali na COCOBA. Ziara hii itawafungua sana.”
Akielezea kwa bashasha Katibu wa Kamati ya Usimamizi wa miradi ya vikundi (“Village Livelihood Committee” (VLC) kijiji cha Mang’ula, Hamisi Dule alibainisha imani kubwa waliyonayo kuhusu Mradi wa REGROW na namna unavyokwenda kubadili maisha yao na kuongeza kuwa kupitia Mradi wamejifunza mambo mengi mazuri na kupitia ziara hiyo wataendelea kujifunza vitu vingi kwani ni dhahiri kuwa sekta ya utalii kwa upande wa Kaskazini mwa nchi yetu imepiga hatua kubwa ukilinganisha na upande wa kusini tulikotoka.
Aidha, Bw.Dule aliishukuru Serikali kwa fursa waliopata na ziara hiyo ya mafunzo.
Mradi wa REGROW unatekelezwa kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani Milioni 150 kutoka Benki ya Dunia.