Na Kassim Nyaki, Ngorongoro Arusha.
Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wametembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ikiwa ni utekelezaji wa kampeni yao ya kutangaza vivutio vya utalii katika Nchi wanachama za Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa Kamati ya kilimo, utalii na Maliasili wa Bunge la Afrika mashariki Mhe. Françoise Uwumukiza ambae ni Mbunge kutoka nchini Rwanda ameeleza kuwa Bunge hilo limeamua kuunga mkono jitihada za Serikali kutangaza utalii na wameamua kuanzia hifadhi ya Ngorongoro kama moja ya maeneo maarufu duniani kwa vivutio vya Utalii.
“Serikali ya Tanzania na uongozi wa Ngorongoro wamefanya kazi nzuri kuhifadhi, kutunza mazingira, kulinda Wanyamapori, mali kale na utalii wa jiolojia ambazo zimepelekea hifadhi ya Ngorongoro kutambulika na UNESCO kama eneo la urithi wa dunia kwa kuwa na hadhi 3 za kimataifa”. Ameeleza Mhe. Owumukiza
Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Utalii na usimamizi wa Wanyamapori Mhe. Dkt. Shogo Mlonzi ambae ni Mbunge kutoka Tanzania ameeleza kuwa takwimu zinaonyesha Nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka 2019 zilivutia watalii milioni 6.95 pekee waliotembelea vivutio vya utalii vilivyoko katika Nchi hizo, hivyo Wabunge wa EALA wameamua kuungana kwa pamoja kutangaza vivutio vilivyopo katika nchi zao ili kuvutia watalii wengi zaidi kutoka Mataifa ya Ulaya, Marekeni, Asia na Afrika kwa Ujumla .
“Tumenzia Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ina utajiri wa vivutio vya utalii ambavyo ni fahari katika nchi yetu, Ngorongoro iko Arusha na Arusha ndio makao makauu ya Bunge la Afrika mashariki, tutaendelea kuwatumia waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi kutembelea vivutio vya utalii kwa kila nchi mwanachama tukiwa katika shughuli za Bunge” amefafanua Mhe. Mlonzi.
Mhe. Balozi Fatma Ndangiza kutoka Nchini Uganda ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutoa kipaumbele katika shughuli za Uhifadhi wa Wanyamapori, mazingira na historia ya urithi wa utamaduni ambao umeendelea kushawishi wageni kutoka mataifa mbalimbali kutembelea Tanzania.
Mwakilishi wa kamishna wa Uhifadhi NCAA Kamishna msaidizi mwandamizi Mhandisi Joshua Mwankunda ameeleza kuwa, ujio wa kundi la Waheshimiwa Wabunge wa EALA ni muendelezo wa NCAA kupokea makundi ya Wageni kutoka mataifa mbalimbali na kusisitiza kuwa…
“Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro linawawezesha wageni kuona vivutio vingi kwa pamoja ikiwepo mandhari asilia (Nature), Utamaduni, vivutio vya jiolojia, wanyama wakubwa watano (Big five), Makumbusho ya Olduvai, Nyayo binadamu wa Kale Laetoli zenye umri wa miaka Milioni 3.6, mchanga unaohama na vingine vingi.
Ujumbe wa Wabunge hao unajumuisha Nchi Saba (7) zinazounda Umoja wa Afrika mashariki ambazo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan ya Kusini na Rwanda.