Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kulia) na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Marco Lombardi (kushoto), wakisaini hati ya makubaliano ya msaada wa Euro 410,000 (sawa na shilingi bilioni 1 za Tanzania) uliotolewa kupitia shirika lake la Maendeleo (AICS), kwa ajili ya programu ya kuimarisha mfumo wa takwimu na usajili wa wananchi ambayo itawezesha Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kusajili watoto 348,391 wenye umri chini ya miaka mitano katika kata 245, zilizoko katika Wilaya 11 za mkoa wa Tanga kupitia vituo 650 vitakavyotumika kusajili watoto hao. Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kulia) na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Marco Lombardi (kushoto), wakionesha hati ya makubaliano ya msaada wa Euro 410,000 (sawa na shilingi bilioni 1 za Tanzania) baada ya kusaini makubaliano hayo kwa ajili ya programu ya kuimarisha mfumo wa takwimu na usajili wa wananchi ambayo itawezesha Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kusajili watoto 348,391 wenye umri chini ya miaka mitano katika kata 245, zilizoko katika Wilaya 11 za mkoa wa Tanga kupitia vituo 650 vitakavyotumika kusajili watoto hao. Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa tatu kulia) na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (wa tatu kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Serikali hizo mbili baada ya kusaini hati ya makubaliano ya msaada wa Euro 410,000 (sawa na shilingi bilioni 1 za Tanzania) kwa ajili ya programu ya kuimarisha mfumo wa takwimu na usajili wa wananchi ambayo itawezesha Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kusajili watoto 348,391 wenye umri chini ya miaka mitano katika kata 245, zilizoko katika Wilaya 11 za mkoa wa Tanga kupitia vituo 650 vitakavyotumika kusajili watoto hao. Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban (wapili kulia), Kiongozi wa Wakala wa Italia wa Ushirikiano wa Kimaendeleo (AICS), Bw. Paolo Razzini (wa kwanza kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Dkt. Amina Msengwa (wapili kushoto), na Mkuu wa Kikosikazi cha Maandalizi ya Maonesho ya Roma 2030, Bw. Gaetano Castellini (wa kwanza kushoto).
…….
Na. Joseph Mahumi, WFM, Dar es Salaam
Tanzania na Italia, kupitia Shirika lake la Maendeleo (AICS), zimetiliana saini mkataba wa msaada wa Euro 410,000 (sawa na shilingi Bilioni 1) kwa ajili ya programu ya kuimarisha mfumo wa takwimu na usajili wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano mkoani Tanga.
Mkataba huo umetiwa saini katika Ofisi za Hazina Ndogo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipangona Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi, kwa niaba ya Serikali ya Italia.
Akiongea baada ya kusaini mkataba huo, Dkt. Natu Mwamba, alisema kuwa msaada huo utawezesha Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kusajili watoto 348,391 wenye umri chini ya miaka mitano katika kata 245, zilizoko katika Wilaya 11 za mkoa wa Tanga kupitia vituo 650 vitakavyotumika kusajili watoto hao.
Dkt. Mwamba aliishukuru Italia kwa ushirikiano mkubwa wa kimaendeleo ambapo hivi karibuni nchi hizo mbili alisema kuwa, nchi hizi mbili zimesaini mkataba wa mkopo nafuu wa Euro milioni 19.7 ambao umechanganywa na msaada wa Euro laki 2 kwa ajili ya kuboresha vyuo vya elimu ya juu vya ufundi ikiwemo, Chuo cha Ufundi Arusha, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia-Karume, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya na Taasisi ya Teknolojia – Dar es Salaam.
“Hii ni miongoni mwa misaada ambayo Italia imeipatia Serikali yetu kwa ajili ya kusaidia sekta mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambapo Serikali hiyo ilitoa msaada wa Euro 170,000 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ofisi na samani” aliongeza Dkt. Mwamba.
Kwa upande wa Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Marco Lombardi, alisema kuwa, Serikali ya Italia kupitia Shirika lake la Maendeleo (AICS), inathamini uhusiano wake na Tanzania na inadhamiria kuwekeza zaidi kwenye uchumi wa buluu, sekta ya kilimo hasa cha umwagiliaji, kuwezesha wanawake kwa kuwa maendeleo ya Tanzania ndiyo maendeleo ya Italia.
“Serikali ya Tanzania inaonesha mwamko katika kusimamia uchumi kupitia Rais wake Mhe. Dkt. Samia Suliuhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Sisi Italia tutazidi kuunga mkono juhudi hizi ili kufanikisha maendeleo ya nchi hii na uhusiano wa nchi hizi” alisema Mhe. Lombardi.
Naye, Kiongozi wa Shirika la Kimaendeleo (AICS), Bw. Paolo Razzini, alisema kuwa, makubaliano hayo yatatekelezwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na wao watatoa msaada zaidi katika kuhakikisha mfumo wa takwimu unaleta matokeo chanya ili kusaidia maendeleo ya haraka kwa watanzania.
“Kama mnavyojua Takwimu ni jambo la muhimu sana katika karne ya 21 na takwimu inaitafanya Serikali ifanye maamuzi sahihi juu ya sera sambamba na idadi ya watu” alisema Bw. Razzini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Dkt. Amina Msengwa, alisema kuwa lengo la mkakati huo ulikuwa kuhakikisha huduma za RITA zinapatikana maeneo karibu na wananchi, kuanzia katika vituo vya afya ambacho watoto wanazaliwa, katika ofisi za Serikali za Mtaa pamoja na Kata, ambapo kutakuwa na mifumo ambayo itahakikisha vyeti vinapatikana kwa urahisi bila vikwazo.
“Mradi huu ni hatua kubwa kwa RITA, ambapo hadi kufikia 2030 tunategemea watoto wote waliopo chini ya umri wa miaka 5, tuwe tumewasajili na tumewapatia vyeti kwa asilimia 100 na kwa sasa tunahakikisha mifumo inakaa sawa ili irahisishe huduma zetu kidigital kupitia mfumo wa e-rita” alisema Dkt. Msengwa.
Hafla hiyo ya kusaini makubaliano ya msaada huo ilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, Kamishna wa Fedha za nje kutoka Wizara hiyo Bw. Rished Bade, Wawakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Sheria na Katiba, Wawakilishi kutoka Roma Italia na Maafisa wengine wa Serikali ya Tanzania.