TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kumpata mwanafunzi wa kidato cha tano mchepuo wa PCB katika Shule ya Sekondari Pandahili ESTER NOAH MWANYILU [18] Mkazi wa Forest Jijini Mbeya aliyekuwa amepotea tangu Mei 18, 2023
Mwanafunzi ESTER NOAH MWANYILU amepatikana Juni 23, 2023 majira ya saa 05:30 asubuhi huko maeneo ya Ifisi katika Mji Mdogo wa Mbalizi baada ya timu ya makachero ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kufuatilia taarifa mbalimbali zilifanikisha kumpata mwanafunzi huyo akiwa katika chumba cha kupanga cha mwanamke aitwaye AZURAT ABDUL @ MOHAMED [24] Mfanyabiashara wa Genge na Mkazi wa Ifisi – Mbalizi.
Kwa mujibu wa maelezo ya AZURATI ABDUL ni kuwa binti huyo aliletwa kwake na kijana mmoja anayemfahamu kwa jina la Baba Jose ambaye ni mteja wake wa kumletea Mkaa kwa Magunia hapo Gengeni kwake.
Alipomleta takribani wiki mbili zilizopita alimueleza kuwa huyo ni mke wake ametoka mkoani Morogoro hivyo anamuomba ampe hifadhi wakati yeye akitafuta chumba cha kupanga na mara atakapopata chumba atakwenda kumchukua.
Binti huyo Alijitambulisha kwa AZURAT ABDUL kwa jina moja la ERICA na kwamba anatokea Morogoro.
Awali Mei 18, 2023 majira ya saa 02:00 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipata taarifa za kupotea kwa mwanafunzi huyo na kuanza uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwahoji viongozi wa Shule hiyo, wanafunzi wenzake, majirani na wale wote waliokuwa wametajwa akiwaomba msamaha kwa maamuzi aliyoyachukua kupitia ujumbe wa maandishi aliouacha mwanafunzi huyo kabla ya kutoweka shuleni hapo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hili ikiwa ni pamoja na msako wa kumtafuta mtuhumiwa aliyekuwa akiishi naye.
Imetolewa na:
BENJAMIN KUZAGA – ACP Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya.