Na Mwandishi wetu, Mirerani
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Civil Social Protection Foundation (CSP) limepongezwa kwa namna linavyojitoa, kuwajengea uwezo na kuwekeza kwa jamii.
Msaidizi wa kisheria (paralegal) wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Nuru Mkireri akizungumza kwenye warsha ya siku nne ya mradi wa Tanzanite kwa uchumi imara wa mwanamke ulioandaliwa na CSP na kufanyika ukumbi wa Mazubu Grand Hotel mji mdogo wa Mirerani.
Mkireri amesema CSP imekuwa msaada mkubwa kwa jamii kwa kuhakikisha wanawajengea uwezo na kupata haki zao za msingi katika maisha yao.
Amesema awali wasaidizi wa kisheria wa eneo hilo walikuwa wanafanya kazi kwa wakati mgumu kutokana na kukosa chumba cha ofisi ila kupitia CSP wamepatiwa ofisi hivi sasa.
“Hivi sasa tuna ofisi kwenye kata ya Mirerani tukifanya kazi zetu kwa ufanisi zaidi hivyo tunawashukuru mno CSP,” amesema Mkireri.
Mwandishi wa habari mwandamizi wa mkoa wa Manyara, Joseph Lyimo amewapongeza CSP kwa kuanzisha mradi huo wa Tanzanite kwa uchumi imara wa mwanamke kwani imebadili changamoto za wanawake wadau wa madini hayo.
Lyimo amesema mwanzo wa mradi huo CSP kupitia Mkurugenzi wake Nemency Iriya na mwanasheria wao Eliakim Paulo waliwakutanisha wajasiriamali wanawake hao na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera na viongozi wa ukuta na kuzungumza changamoto zinazowakabili na sasa zimefanyiwa kazi.
“Tumesikia hapa kuwa hivi sasa wanawake wanapekuliwa kwa stara kwenye lango la kutoka tofauti na awali walipokuwa wanavuliwa hadi nguo za ndani kwa kweli kupitia mradi huu CSP wanastahili kupongezwa,” amesema Lyimo.
Kaimu Ofisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani Isack Mgaya akifungua warsha hiyo ameipongeza CSP kwa kumetoa mchango mkubwa kwa jamii kwa kuwajengea uwezo na kumaliza changmoto mbalimbali.
“Hongereni sana CSP mnafanya kazi nzuri na ya yenye kuacha alama hasa kupambana na changamoto zilizokuwa zinawakabili wanawake wanaofanya shughuli zao ndani ya ukuta unayozunguka migodi ya madini ya Tanzanite vikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia,” amesema Mgaya.
Mwanasheria wa CSP Eliakim Paulo amesema lengo la warsha hiyo ni wanawake wajasiariamali, wasaidizi wa kisheria na waandishi wa habari kuwajengea uwezo wa kuweza kuripoti changamoto zinazowakabili wakiwa kwenye shughuli zao.
Eliakim amesema uchumi wa Mirerani unabebwa na madini ya Tanzanite ambayo yanachimbwa na wanaume lakini masuala ya kijamii haswa familia, yanabebwa na wanawake wajasiriamali.
Eliakim amesema kuwajengea uwezo wanawake katika masuala mbalimbali yanayowahusu hasa suala la kiuchumi ni kuiokoa jamii ya Mirerani na kuwaokoa watoto ambao ndiyo Taifa la kesho.
Mwezeshaji wa warsha hiyo Kaimu Mkurugenzi wa shirika la biashara na haki za binadamu Tanzania (BHRT) Rose Ugulumu ametoa mada mbalimbali za kuwawezesha washiriki wake, ikiwemo haki za binadamu na ujasiriamali
Ugulumu amesema tatizo la jamii kukosa elimu ya moja kwa moja juu ya masuala ya uwekezaji, haki zao pamoja na sheria wanazopaswa kuzifuata na kwamba ifike mahali jamii izingatie na kujikumbusha sera za ujamaa na kujitegemea iliyoasisiwa na viongozi wa nchi.
“Hapa kuna machimbo ya madini ya Tanzanite hivyo wanawake na jamii kwa ujumla wanapaswa kunufaika na pia serikali iwekeze huduma za afya na nyingine ili wadau wanufaike.