Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Umma Charles Shirima kutoka Mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana (CMSA)
Washiriki wa mafunzo wakiwa Ukumbini
…….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana (CMSA) imetoa elimu kwa vijana Jijini Mwanza juu ya ujio wa miongozo ya mitaji ya alaiki.
Elimu hiyo iliyowakutanisha vijana 100 kutoka sehemu mbalimbali imetolewa leo Ijumaa Juni 23,2023.
Charles Shirima ni Meneja wa uhusiano na elimu kwa umma kutoka Mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana (CMSA) amesema,lengo la kutoa elimu hiyo ni kuhakikisha vijana wanapata uelewa wa fedha ambao utawasaidia kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Amesema miongozo ya mitaji ya alaiki ni mfumo unaotumia tehama ambayo inawezesha biashara ndogo na za kati kukusanya fedha kutoka kwa umma kwaajili ya kuwekeza.
” Kama tunavyofahamu biashara ndogo na za kati zinakuwa hazina sifa za kuorodheshwa kwenye soko la mitaji au mikopo kutoka benki kwahiyo mitaji ya alaiki ni jukwaa linalowezesha biashara hizo kupata fursa ya kukusanya mitaji kutoka kwa umma”, amesema Shirima
Ameeleza kuwa kwa hapa Tanzania mitaji ya alaiki bado ni jambo geni lakini katika nchi zingine limeanza hivi karibuni,kulingana na mazingira ya hapa nchini ongezeko la uhitaji wa matumizi ya jukwaa hilo ni kubwa ndio maana tumeshirikina na wadau wengine wa sekta ya fedha kwaajili ya kuandaa miongozo ya kuyawezesha majukwaa hayo kupata leseni za kuendesha shughuli zao.
Kwa upande wake Afisa mpango na masuala ya fedha kutoka Shirika la kuhudumia viwanda vidogo Sido Mkoani hapa Salum Daniford, amesema wamekuwa wakiwalea vijana mbalimbali kwenye fursa za fedha ili kuwawezesha kutunisha mifuko yao.
Tunapotoa mafunzo kwa vijana tunategemea waje wawe wajasiriamali wakubwa ambao watamiliki Makampuni yatakayosafirisha bidhaa ndani na nje ya nchi.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Mamlaka hiyo kwakuwapa mafunzo ambayo yatawasaidia kwenye biashara zao huku wakiwaomba kuwafikia vijana wengi zaidi hapa nchini ili waweze kupata elimu hiyo.