NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Pamoja na mipango mbalimbali inayofanywa na Mamlaka na Taasisi zinazohusika na uhifadhi, kukabiliana na uharibifu wa mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji, bado uharibifu ni mkubwa unaosababishwa na uazishwaji wa mashamba mapya, ukataji wa Miti pamoja na ufugaji wa mifugo mingi kwenye eneo dogo.
Katika kuhakikisha vyanzo vya Maji vinalindwa na kuhifadhiwa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu kwa kushirikiana na Mamlaka na Taasisi zinazohusika kwenye uhifadhi, zimefanya ziara ya kukagua chanzo cha Mto Morogoro kuona kiini cha uharibifu wa mazingira kwenye chanzo hicho.
Msimamizi wa Mzingira Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Morogoro (MORUWASA) Mhandisi Rashidi Bumarwa, amesema Mto Morogoro ni kati ya vyanzo vikubwa vinavyotegemewa na MORUWASA kusaidia upatikanaji wa Maji katika Mji wa Morogoro.
“Tumeona kuna baadhi ya watu wamechepusha Maji, hii inatusababisha kupungua kwa maji kwenye mitambo yetu, ziara hii ambayo tumeungana na wadau mbalimbali inalengo la kuangalia uharibifu wa mazingira, baadae tuje na mpango kazi utakao tuongoza katika kudhibiti uharibifu.” Alisema Bumarwa.
“Kama tunavyoona Maji yanatoka juu yakiwa safi na salama lakini kadri yanavyozidi kushuka chini yanaanza kupungua ubora, hii ni inasababishwa na shughuli za kibinaadamu zinazoendelea ndani ya hifadhi ya vyanzo vyetu vya maji hasa kilimo”. Aliongeza.
Mwakirishi kutoka Baraza la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Morogoro- Rufiji Mhandisi Jenne Kadoda amesema, Sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni ya 57(1) inakataza shughuli za kibinaadamu kwenye vyanzo vya maji na inapendekeza shughuli ziazie mita 60.
Amesema pamoja na sheria hiyo kuruhusu shughuli za kibiaadamu kufanyika nje ya Mita 60 ya chanzo cha Maji, Baraza la Mazingira huwa linaangalia umuhimu wa chanzo husika kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
“Mita 60 ni umbali wa kuazia, umbali ule unatakiwa zaidi chanzo huwa kina hifadhia mpaka mita 200 kutokana na ukubwa na umuhimu wake”. Alisema Kadoda
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Choma kata ya Mlimani Manispaa ya Morogoro Dismiss Marco amesema zoezi la uhifadhi limekuwa shirikishi katika mtaa wake na kwamba wamekuwa wakipanda Miti kwenye kingo za Mto pamoja na kulinda hifadhi ya vyanzo vya Maji.
“Mwezi uliopita tulipata miti zaidi ya 200 kutoka Wami- Ruvu, tulipanda kwenye kingo za mito ikiwa ni sehemu ya uhifadhi wa vyanzo vya maji”. Alisema Mwenyekiti wa Mtaa wa Choma.
Ziara hiyo imehusisha wataalamu mbalimbali kutoka Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Morogoro, Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Wakala wa Misitu Tanzania, Manispa ya Morogoro pamoja na Skauti Wilaya ya Morogoro.