Wakati wimbi la vijana wasiyo na ajira nchini likizidi kuongezeka kila mwaka kutokana na kuhitimu mafunzo ya elimu ya juu katika vyuo vikuu na vyuo vya kati ,Mbunge wa Lupembe Edwin Enos Swale ameiomba serikali kupitia tume mpya ya mipango iliyoundwa hivi karibuni kuanza mpango wa lazima wa kufufua viwanda viwanda vilivyokufa kote nchini.
Akizungumza wakati akichangia bajeti ya 2023/24 ya srikali Mbunge Swale amesema kwa uwezo wa serikali haina uwezo wa kuajiri watu wote wanaingia kwenye soko la ajira ni vyema ukafanyika mpango wa kufufua viwanda kikiwemo Kiwanda cha Maziwa cha Njombe ,Kiwanda cha Olivado na kisha kuimarisha viwanda vya chai vinavyosuasua mkoani Njombe ili kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wengi.
Swale amesema takwimu zilizopo zinaonyesha watu milioni moja huingia kwenye soko la ajira kila mwaka ili hali ilani ya chama imeahidi kutoa ajira mil 8 kila mwaka jambo ambalo linashindikana na kuishia kuajiri watu elfu 70 tu hivyo serikali ichukua hatua za lazima za kukabiliana na chaangamoto ya ajira kwa kufufua sekta ya viwanda.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo wa Lupembe ameitaka serikali kuondoa sintofahamu iliyopo sasa kwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya kutosafirisha nje na kisha kuiomba serikali kuacha wakulima kuendelea kuuza mazao yao hususani mahindi popote bila kikwazo ili kutanua wigo wa soko kwasababu vikwazo hivyo vimekuwa chanzo cha kuporomoka kwa bei ya mazao.
Amesema tangu kuibuka kwa taarifa za zuio la kusafirisha mazao kumesababisha bei ya mahindi kushuka kutoka shilingi elfu 15 hadi elfu 5 katika vijiji vya Mtwango,Ikondo,Igombola na Ikuna vilivyopo jimbo la Lupembe wilayani Njombe na kisha kuomba wakulima kuachwa huru kuuza popote mazao yao kwani kufanya hivyo kunaathiri wakulima.
Aidha Swale amezungumzia changamoto inayowakuta wafanyabiashara kutoka kwa maofisa wa TRA magetini,Urasimu katika utoaji wa leseni za biashara na vibali huku pia akitaka serikali kutoa bei elekezi za mazao kwa wakulima sambamba na kuungezea fedha wakala wa chakula nchi NFRA ili uweze kununua mazao mengi kwa wakulima.
Mbali na suala la ajira,biashara ya mazao na urasimu katika utoaji wa vibali mbunge huyo wa Lupembe pia ameiomba serikali kupitia bajeti mpya ya serikali ya mwaka 2023/24 kuanza ujenzi wa barabara ya Kibena-Lupembe hadi Madeke kwa kiwango cha lami kama ahadi ilivyokuwa imetolewa na serikali kwa nyakati tofauti na kukata kiu ya wananchi.
Kwa upande wake Hussen Bashe ambaye ni waziri wa kilimo nchini akifafanunua kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali katika sekta ya kilimo ni pamoja na kufungua vituo vya kununua mazao katika wilaya zote nchini huku pia akisema tayari wakala wa chakula wa taifa NFRA umeanza kununua mahindi ya wakulima kwa bei ya shilingi 600 hadi 700.
Kuhusu mfumo wa kutoa vibali vya kusafirisha mazao nje ya nchi Waziri Bashe amesema kuanzia julai mosi serikali itaanza kutoa leseni kupitia mtandao ili kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara hatua ambayo itaongeza fursa kwa wakulima ya kuuza mahindi.