Balozi wa India nchini Tanzania Mhe Binaya Srikanta Pradhan akitembelea na kuangalia shughuli zinazofanywa kwenye Hospital ya Taifa ya Rufaa ya Wanyama iliyopo Chuo Kikuu cha SUA Mjini Morogoro.
Balozi wa India nchini Tanzania Mhe Binaya Srikanta Pradhan akizungumza na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SUA Prof. Raphael Chibunda alipofanya ziara chuoni hapo hivi karibuni.
Balozi wa India nchini Tanzania Mhe Binaya Srikanta Pradhan akitembelea na kuangalia shughuli zinazofanywa kwenye Hospital ya Taifa ya Rufaa ya Wanyama iliyopo Chuo Kikuu cha SUA Mjini Morogoro.
…………………………..
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro kimekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini Tanzania Mhe. Binaya Srikanta Pradhan kuhusu kushirikiana katika maeneo ambayo yatanufaisha Tanzania na India hususani katika Teknolojia kwa ajili ya kilimo pamoja na Tehama, Tafiti na kujengeana uwezo.
Hayo yamebainishwa mkoani Morogoro wakati wa ziara ya Balozi huyo wa India nchini Tanzania chuoni hapo na kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Wanyama pamoja na eneo la Uchumi wa Buluu.
Mhe. Balozi Srikanta Pradhan amesema amefurahishwa kuona SUA inavyofundisha na kuwaandaa vyema wanafunzi katika kujiajiri na pia inavyoshirikiana vyema na jamii.
India wamekipa kipaumbele kilimo hivyo kwa kushirikiana na Tanzania kupitia SUA wataweza kuboresha katika kilimo.
“SUA inafanya kazi vizuri hasa katika maeneo yanayoihusisha jamii moja kwa moja hivyo ushirikiano wao utalenga katika kutatua changamoto ambazo jamii zao zinakumbana nazo hasa kwenye Sekta ya kilimo hivyo naamini tutaenda kushirikiana katika utatuzi wa changamoto hizo kwa kuwa na Programu za pamoja lakini pia Miradi mbalimbali”, alisema Mhe. Binaya Srikanta.
Kwa upande wake Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema uhusiano ambao wameingia na Serikali ya India ni sehemu tu ya mahusiano ambayo wapo nayo hivyo moja kati ya makubaliano ambayo wameyafanya ni kuhusiana na Tafiti hasa zinazohusiana na matatizo yanayowakabili nchi zote mbili ikiwemo magonjwa ambukizi kwa binadamu na hata Wanyama na hiyo ni kutokana na kuwepo kwa pamoja katika ukanda wa Kitropiki.
Vilevile wamekubaliana kupeleka timu ya wataalam wao kwenda kujifunza na kuangalia Mitaala yao, namna wanavyofundisha na kuwaandaa wahitimu wao ili na wao wahitimu wao ikiwezekana kwa sehemu kubwa wawe na umahiri unaokaribiana na wahitimu wengi wa Vyuo Vikuu vya India hasa katika maswala ya Teknolojia hasa kwenye swala la Tehama ambapo India wamekuwa wakifanya vizuri.
“Wahitimu wao wengi mawazo yao yameshatoka kwenye kumaliza Chuo na kwenda kuajiliwa, wengi wanafikiria kujiajiri, kuingia kwenye biashara na uzalishaji na sisi uko ndiko tunapotaka kuelekea ndio maana mkazo wa ushirikiano wetu ni katika maswala ya ujasiriamali”, amesema Prof. Chibunda.
Ameongeza kuwa, kutokana na India kuwa soko kubwa la mazao yanayolimwa Tanzania wamekubaliana kushirikiana na Taasisi mbalimbali za India, Ubalozi wake na Serikali yake katika kuwafundisha wakulima wa Kitanzania njia bora ya kulima hayo mazao ambayo soko la India wanayahitaji sana ili yanapo vunwa kuwepo na njia bora ya kuyahifadhi ili yafike bila kikwazo cha upungufu wa ubora.