Na. Jacob Kasiri- Ruaha.
Balozi wa hiari wa Utalii nchini na mwana-mitandao ya kijamii (social media) inayofuatiliwa sana duniani Nicholas Reynolds almaarufu Bongozozo amekoshwa na kuvutiwa na Utalii wa Puto “Balloon safaris” ikiwa ni moja ya zao la utalii lililoanzishwa takribani miongo miwili iliyopita katika Hifadhi ya Taifa Ruaha na kuahidi kwenda kuhamasisha watalii wengi zaidi kutembelea hifadhi hiyo ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano alizozianzisha kupitia Filamu ya The Royal Tour ambayo imeendelea kuvuta watalii wengi zaidi kuja nchini.
Akiwa ndani ya hifadhi hiyo leo tarehe 21.06.2023 Bongozozo amesema, “nimekoshwa na kuvutiwa sana na utalii wa puto, nikiwa juu nimeona mandhari nzuri ya “The Great Ruaha River”, wanyama kama vile Tembo, Duma, Swala, Kudu, Mamba, Viboko na pia, nimeona miti aina ya Mibuyu iliyopukutisha majani kipindi hiki cha kiangazi na kufanya matawi yake yaonekane mithiri ya mizizi”. (Tunaweza kusema kwa kutania, “Mibuyu ni miti mizizi juu”).
Aidha, watalii hao waliposhuka kutoka kwenye puto “Balloons” walipewa “champagne” ikiwa ni ishara ya mapatano kati ya “baloon Captain” na mahali inaposhukia “baloon” na baadae majira ya saa 4:30 asubuhi watalii hao wakichagizwa na Bongozozo walipata kifungua kinywa kizito (heavy breakfast) katika mazingira ya asili yaani (Bush meal), lengo la milo hiyo uwapo Hifadhi ya Taifa Ruaha ni kukonga mioyo ya wageni, kuona wanyama kwa ukaribu huku ukindelea kuburudika na pia, inasemekana kuwa kisaiklojia ulapo chakula porini huku ukisikia sauti za ndege, mlo huwa mtamu na kuineemesha nafsi.
Pia katika kuvitambua na kunadi mazao ya utalii Bongozozo amefanya utalii wa kutembea kwa miguu, lengo likiwa ni kuona vivitio vya utalii ambavyo havionekani unapokuwa ndani ya gari na kujifunza vitu vingi ambavyo watalii wengine huvipuuzia kama vile nyayo za wanyama, pamoja na vinyesi vyao. Kwa mfano vinyesi hivyo hutoa tafasiri nyingi kwa wanyama wenzao.
Watalii hao wakiongozwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) wamefanya utalii wa kuvua samaki (sport fishing). Kwa Hifadhi ya Taifa Ruaha samaki anayevuliwa ni mchena aina ya Hydrosinus tanzaniae ambaye hupatikana Tanzania tu, Mchena huyu hutofautiana na Michena wengi kwa kuwa na rangi ya bluu mkiani (Blue adipose fin).
Akiwa jijini Arusha wiki mbili zilizopita, Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Mohamed Mchengerwa (mb) alisema wizara yake itashirikiana na mwanamitandao huyo katika kuvitangaza vivutio vya utalii kimataifa kama anavyofanya katika Marathon mbalimbali za kimataifa kwa kupeperusha bendera ya Tanzania na kuuliza maswali mbalimbali yanayohusiana na vivutio vya utalii vilivyoko Tanzania.
Naye Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi Amina Salum – Mkuu wa Idara ya Utalii Hifadhi ya Taifa Ruaha, ameishukuru wizara, TTB na Mwanamitandao huyo kwa kuungana na TANAPA kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na Kusini kwa ujumla na kuahidi kushirikiana nao ili kuvutia watalii wengi zaidi.