NA K-VIS BLOG, ZANZIBAR
MFUKO
wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekabidhi vifaa tiba kwa
vituo vya afya, Mkunguni na Dimbani, Wilaya ya Kusini Unguja, Zanzibar, ikiwa
ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Tanzania
huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kila
inapofika Juni 23 ya kila mwaka ili kutambua mchango wa Watumishi wa Umma
katika Maendeleo ya taifa lolote duniani.
Hapa
nchini maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yameanza Juni 16 na yatafikia
kilele Juni 23, 2023 ambapo kwa mwaka huu yanabeba kauli mbiu isemayo
“Kufanikiwa kwa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (Acfta) Kunahitaji
usimamizi wa Utumishi wa Umma Wenye Mtazamo wa Kikanda”
Akizungumza
mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice
Musa-Lupi ambaye alifuatana na Meneja wa PSSSF Zanzibar, Bi. Amina Kassim na
Meneja Utawala Bi. Gloria Mboya, alisema Mfuko umeamua kuadhimisha siku ya Utumishi wa Umma kwa kutoa msaada wa vifaa tiba kwa vituo
hivyo vya afya kwa kuthamini mchango mkubwa wa watumishi wa umma katika kuleta
maendeleo na ustawi katika jamii yetu.
“Vifaa
tiba tulivyokabidhi leo vitawezesha utoaji huduma bora na za hali ya juu kwa
wagonjwa wetu, tumetoa vifaa kama vile mashine za kupima, vifaa vya kuimarisha
usafi, vifaa vya kusaidia uchunguzi wa magonjwa, Viti ya matairi (Wheel Chairs)
na vipoza hewa (viyoyozi), ni imani yetu kwamba vifaa hivi vitatumika kwa
ufanisi na kuleta mabadiliko chanya katika afya ya wananchi wetu.” Alifafanua
Alisema
Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), ilitoa maelekezo ya namna nzuri ya Taasisi
za Umma kuadhimisha Wiki hii ya Utumishi wa Umma, kwa kukutana na watumishi
wanaofanya kazi maeneo ya pembezoni ili kujua changamoto wanazokabiliana nazo
katika kuwahudumia wananchi.
Huduma
ya afya ni mojawapo ya mahitaji muhimu ya kila mwananchi na kwamba kwa
kuboresha huduma za afya ni kuimarisha afya ya jamii na kulinda nguvu kazi na
hivyo kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa ujumla, alifafanua Bi. Beatrice.
“Tunahimiza
watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma katika majukumu
yenu ili kuhakikisha kuwa huduma bora za afya zinapatikana kwa kila mwananchi.”
Alisisitiza Beatrice Musa-Lupi.
Alisema
Mfuko unatambua kuwa changamoto za kifedha na rasilimali zinaweza kuwepo,
lakini hatua hiyo ya Mfuko ya kujitolea na kushirikiana na taasisi zingine,
inaweza kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya afya.
“Tunatoa
wito kwa wadau wengine na sekta binafsi kuunga mkono juhudi zetu na kushiriki
katika kuleta maendeleo katika huduma za afya.” Alisisitiza.
Kwa
upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Kusini Unguja Bw. Omar Mohamed Kasongo
aliushukuru Mfuko wa PSSSF kwa misaada hiyo na kusema huduma ni sehemu ya tiba,
vifaa hivyo vitasaidia kuboresha huduma za tiba kwenye vituo hivyo vya afya na
hivyo kuwanufaisha wananchi wa maeneo hayo.
Alisema
pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali zote mbili, Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika
kufanya mapinduzi katika sekta ya afya lakini panapotokea wadau wa kuiunga
mkono serikali linakuwa jambo jema.
“Nawapongeza
kwa kushirikiana na serikali katika juhudi zake za kuboresha huduma za afya.”
Alisema Bw. Kasongo.
Aidha
Mganga Dhamana (Mfawidhi) wa Wilaya ya Kusini Unguja, Dkt. Vuai Ramadhan Mzee,
licha ya kuishukuru PSSSF kwa msaada huo alisema kwao ni jambo la neema sana.
“Wapo
wengi wenye uhitaji wa vifaa kama hivi, kwa kutuona sisi hii ni neema kwetu,
mmekuja kuboresha afya ya wananchi wa Kizimkazi tunawashukuru sana na
msituchoke kwani hii si mara ya kwanza kutusaidia.” Alisema.