Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo ametoa wito kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya Kondoa wanaopakana na Pori la Akiba la Mkungunero, kuheshimu taratibu za kisheria za nchi, na iwapo kuna sheria inayohitaji marekebisho basi utaratibu uliowekwa kufanya mabadiliko ufuatwe.
Katibu Mkuu Chongolo ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kinyasi, Kata ya Kinyasi (Bwawani), baada ya kutembelea ujenzi wa mradi wa Shule ya Msingi Kinyasi, Bwawani, iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi kwa kuchanga shilingi milioni 8 na Serikali kutoa zaidi ya shilingi milioni 490.
Katibu Mkuu alitoa kauli hiyo mara baada ya kupokea malalamiko ya wananchi hao kuhusu mgogoro wa muda mrefu juu ya mpaka wa pori hilo la akiba la Mkungunero.
“Sheria lazima ibaki kuwa sheria na tunapotaka kubadilisha sheria lazima twende kwenye mchakato wa kubadili sheria,” amesema Chongolo.
Katika ziara hiyo yenye lengo la kukagua, kusimamia na kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 pamoja na kuimarisha uhai wa Chama Cha Mapinduzi, Katibu Mkuu ameongozana na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Ndugu Sophia Mjema pamoja na Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndugu Issa Haji Ussi Gavu, ambapo baada ya siku ya Jumatatu Juni 19, 2023 kutembelea maeneo mbalimbali ya majimbo mawili ya Kondoa Vijijini na Kondoa Mjini, katika Wilaya ya Kondoa, leo Jumanne, Juni 20, 2023, aanatarajiwa kuwa Wilaya ya Chemba, ukiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku 8 katika Mkoa wa Dodoma.