Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas (katikati) akizungumza kwenye majadiliano ya mafunzo ya uwasilishaji,usambazaji na uhamasishaji matumizi ya matokeo ya sensa ya watu kwa viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma iliyofanyika kwenye ukumbi wa Parokia ya Bombambili mjini Songea, kulia kwake ni Meneja wa Takwimu Mkoa wa Ruvuma Mwamntumu Athuman Ulega na kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Ndugu Oddo Mwisho.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas mafunzo ya uwasilishaji,usambazaji na uhamasishaji matumizi ya matokeo ya sensa ya watu kwa viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma iliyofanyika kwenye ukumbi wa Parokia ya Bombambili mjini Songea.
baadhi ya wadau mkoani Ruvuma wakiwa kwenye mafunzo ya uwasilishaji,usambazaji na uhamasishaji matumizi ya matokeo ya sensa ya watu kwa viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma iliyofanyika kwenye ukumbi wa Parokia ya Bombambili mjini Songea.
…….
Na Albano Midelo,Songea.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewaasa viongozi na watendaji katika ngazi zote za kiutawala kusimamia vema maendeleo kwa kugawa rasilimali za taifa kwa kufuata vigezo vya kitakwimu na sio upendeleo.
Kanali Thomas ametoa rai hiyo wakati anafungua semina ya uwasilishaji,usambazaji na uhamasishaji matumizi ya matokeo ya sensa kwa viongozi na watendaji kutoka wilaya zote za mkoa wa Ruvuma,iliyofanyika kwenye ukumbi wa Parokia ya Bombambili mjini Songea.
“Rasilimali za Taifa ni za wote hivyo haitakiwi kumpendelea mtu,kundi fulani au eneo fulani,badala yake zinatakiwa kugawanywa kulingana na mahitaji ya watu katika maeneo yao wakiwemo watu wenye ulemavu,wazee,vijana na wajasirimali wadogo wadogo’’,alisema Kanali Thomas.
Amesisitiza matumizi mazuri na bora ya matokeo ya sensa katika kufanya maamuzi yenye kufuata vigezo vya kitakwimu badala ya matakwa binafsi ya baadhi ya watu.
Hata hivyo ameyataja matokeo ya sensa mkoani Ruvuma yanaonesha kuwa idadi ya watu imeongezeka kutoka watu 1,376,891 mwaka 2012 hadi kufikia watu milioni 1,848,794 mwaka 2022 ikiwa ni sawa na ongezeko la watu 471,903.
Amesema matokeo hayo yanadhihirisha kuwa kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu kimeongezeka kutoka asilimia 2.1 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 2.9 mwaka 2022 ikiwa ni chini ya kiwango cha kasi ya ongezeko la idadi ya watu kitaifa ambacho ni asilimia 3.2 kwa mwaka 2022.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa,matokeo ya sensa mkoani Ruvuma yanaonesha kuwa watu 471,903 wameongezeka katika kipindi cha miaka kumi kutoka mwaka 2012 hadi 2022.
Kutokana na matokeo hayo ya sensa,Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa viongozi na watendaji kuhakikisha kuwa mipango yote ya maendeleo ya muda mfupi,muda wa kati na muda mrefu inawekwa kwa kuzingatia idadi ya watu,mahitaji yao na hali halisi ya mazingira.
Awali taarifa ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt.Albina Chuwa iliyosomwa kwa niaba yake na Meneja wa Takwimu Mkoa wa Ruvuma Mwantumu Athuman kwenye mkutano huo,imeeleza kuwa utekelezaji wa sensa ya watu na makazi umefanyika katika awamu tatu.
Amezitaja awamu hizo kuwa ni maandalizi,zoezi la kuhesabu watu na uchakataji, uchambuzi wa taarifa zilizokusanywa,uandishi wa ripoti za matokeo ya sensa na usambazaji na mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa.
Amesema hivi sasa idara ya takwimu inaendelea na awamu ya tatu ya semina na mafunzo ambayo ilianza mara tu baada ya kumalizika zoezi la kuhesabu watu ambapo ameitaja mikoa ambayo imeshapata mafunzo hayo ni Dodoma,Kigoma, Dar es salaam,Lindi,Mtwara,Pwani na Ruvuma.
Mada ambazo zimetolewa kwenye mafunzo hayo ni matumizi ya matokeo ya sensa na mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi na watendaji mkoa wa Ruvuma.
Mada nyingine ni matokeo ya sensa ya Mkoa wa Ruvuma kwa ramani,mwongozo wa kitaifa wa usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya mwaka 2022 na mfumo wa upatinaji wa matokeo ya sensa kidijitali.
Wakizungumza baada ya kupata mafunzo hayo,Mwakilishi wa Vyama vya Siasa mkoani Ruvuma Elias Nchimbi na Mwakilishi wa Viongozi wa Dini Rajabu Songambele ambaye pia ni Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Ruvuma wameishukuru serikali kwa kuwashirikisha katika hatua zote za sensa ya watu na makazi hali ambayo imejenga hamasa kubwa ya matumizi ya takwimu katika jamii.