DIWANI wa Kata ya Chandama kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mohamed Mgongaji amemueleza Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo jinsi anavyotekeleza Ilani ya CCM, tangu alipochaguliwa uchaguzi mkuu uliopita.
Akizungumza katika mkutano wa shina namba moja la CCM, Tawi la Chandama, kwa Balozi Fatuma Hamis Dutuka, mbele ya Katibu Mkuu Chongolo aliyefika katika kata hiyo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika majimbo yote ya Mkoa wa Dodoma yenye lengo la kusikiliza changamoto za wananchi, kuhamasisha uhai wa Chama, kukagua miradi ya maendeleo na utekelezaji wa Ilani ya CCM, Mhe. Mgongaji alisema kuwa yeye kama diwani baada ya kuchaguliwa alianza kutekeleza Ilani ya CCM, ikiwemo kusimamia miradi ya maendeleo katika kata hiyo.
“Kwa sababu miradi iliyoko ni ya Ilani ya Chama Cha Maapinduzi na lazima nisimamie mimi kama diwani, nimesimamia miradi mingi ambayo imeshatekelezwa na imekamilika. Baadhi ya inayosuasua ni pamoja na miradi ya maji hiyo ndiyo changamoto kubwa mpaka sasa hivi, tunategemea Katibu Mkuu umekuja hili utalichukua angalau tuweze kuona hii changamoto hapa inaishaje,” amesema Diwani Mgongaji.
Akijibu kuhusu suala la changamoto ya kusuasua kwa Mradi wa Maji wa Chandama, Chongolo alitoa siku saba kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufikisha na kuwasha umeme katika eneo la mradi, kwani ni mojawapo ya kikwazo kilichotajwa na Wakala wa Maji Vijiji (RUWASA) kushindwa kuchimba visima kutokana na kutokuwepo kwa umeme utakaowezesha mitambo ya uchimbaji, kufanya kazi.
Aidha, aliwaagiza RUWASA ndani ya muda wa majuma matatu wafike mahali ambapo panatakiwa kuchimbwa kisima kwa sababu umeme utakuwa umeshafika, akiwaagiza, wachimbe kisima ambacho wananchi watakitumia wakati RUWASA wakiendelea kutengeneza mtandao wa maji na kukamilisha mradi mkubwa wa maji ambao utasambaza maji katika sehemu kubwa zaidi.