Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja amezitaka taasisi za Wizara ya Maji kushirikiana ili kuondoa adha ya maji kwa wananchi.
Amesema hayo Jijini Mwanza katika kikao cha majumuisho ya ziara ya siku tano. Kikao hicho kimehusisha watendaji kutoka Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA), RUWASA Mwanza na Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria.
“Nimewakutanisha hapa, napenda tuwe kitu kimoja, mnapaswa kutambua kuwa jukumu letu ni moja na nyote mnatekeleza majukumu yenu kwa niaba ya Wizara ya Maji,” Mhandisi Luhemeja alisema.
Alisema kila taasisi inalo jambo la kujifunza kutoka kwenye taasisi nyingine na aliwaelekeza watendaji hao kuandaa utaratibu wa kukutana na kujadili namna bora za kuwafikishia huduma ya majisafi wananchi.
Alisema kupitia ushirikiano huo baadhi ya changamoto zitapata majibu kwa haraka na hivyo kufikia azma ya Serikali ya kumtua Mama ndoo ya maji kichwani huku akitolea mfano kuwa zipo baadhi ya changamoto za MWAUWASA ambazo zinaweza kutatulika kirahisi kwa kushirikiana na RUWASA ikiwa ni pamoja na changamoto ya kufikisha maji maeneo ya pembezoni mwa Jiji.
Alisema Sekta ya Maji inao umuhimu mkubwa kwa jamii na kwamba miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ni kuhakikisha inafanya vizuri.
“Tunafanya kazi zinazogusa maisha ya watu, shabaha yetu kubwa ni kuwapatia Watanzania majisafi, nafsi zetu zidhamirie kuwasaidia Watanzania,” Mhandisi Luhemeja alisema.
Aidha, alisisitiza watendaji hao kujenga mifumo bora ya utoaji huduma na akisisitiza kuwa vijana wajengewe mazingira ya kufanya kazi pamoja na kuwa na utamaduni wa uwazi ilhali kila mmoja akitambua jukumu la msingi, wajibu na lengo mahsusi la majukumu aliyoaminiwa kuyatumikia.
“Msifanye kazi ili mradi tu mnafanya, fanyeni kazi kwa dhamira ya dhati ya kuwasaidia Watanzania waondokane na adha walionayo ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama nanyi mtanufaika na stahiki mtakazopata kutokana na huduma mnayoitoa kwa wananchi,” Mhandisi Luhemeja alisema na kuongeza suala la uwajibikaji na umoja miongoni mwa watumishi ni muhimu, bila hivyo mafanikio hayatoweza kupatikana endapo Menejimenti haitokuwa kitu kimoja.
Akizungumzia suala la upatikanaji wa huduma ya majisafi kwenye baadhi ya maeneo ya pembezoni mwa Wilaya ya Ilemela aliitaka MWAUWASA kutumia matenki yake ya maji ya Buswelu na Igogwe kuhakikisha maji yanafika kwa wananchi.
“Nimetembelea maeneo ya Kata za Kahama, Nyamhongolo na Shibula ni kwamba maeneo yote haya yanaweza kupata huduma kupitia matenki haya, MWAUWASA fikeni huko mshughulikie hili na pia timu ya ufundi izunguke kwenye mitaa yote mnayohudumia kutazama namna bora ya kufikisha huduma kwenye maeneo yenye changamoto,” Mhandisi Luhemeja alielekeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Maji, CPA Joyce Msiru aliwasisitiza watendaji hao kutozoea matatizo ya wananchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA akizungumza kwa niaba ya watendaji wengine alishukuru.
“Tumenufaika na ujio wenu, kupitia uzoefu wako Naibu Katibu Mkuu, tumejifunza mengi kutoka kwako na maelekezo yako tayari tumeanza utekelezaji,” Mhandisi Msenyele alisema.