Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu akizungumza leo tarehe 17/6/2023 katika Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuadhimisho miaka ya 25 ya Mafanikio ya Benki ya NMB
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu akipokea gawio la Serikali kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna leo tarehe 17/6/2023 katika Ukumbi wa Mliman City, Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuadhimisha miaka 25 ya Mafanikio ya Benki ya NMB.
Baadhi ya Washiriki wakiwemo viongozi wa serikali, viongozi wa dini, wafanyakazi wa Benki ya NMB wakiwa katika hafla ya kuadhimisha miaka 25 ya Mafanikio ya Benki ya NMB yaliofanyika leo tarehe 17/6/2023 katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu ameipongeza Benki ya NMB kwa kufanikiwa kuwa kiongozi katika kutengeneza faida katika utekelezaji wa majukumu yake, huku akitoa wito kwa taasisi nyengine za umma kujiendesha kwa ufanisi na ushindani ili kuleta tija kwa Taifa.
Akizungumza leo tarehe 17/6/2023 Jijini Dar es Salaam katika kuadhimisho miaka ya 25 ya Mafanikio ya Benki ya NMB ambayo yamekwenda pamoja na kukabidhi gawio kwa Serikali Shilingi Bilioni 45.5, Rais Dkt. Samia, amesema kuwa serikali inaendelea kufanya jitihadi katika kuhakikisha mashirika yote ya umma yanafanya kazi kwa ufanisi.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa mashirika yasiyo na faida yanashindwa kujiendesha na kuitia hasara Serikali.
“Tutafanya tathmini kupitia Msajili wa Hazina ambapo Serikali itayachukulia hatua na kuyafuta mashirika ambayo hayafanyi vizuri” amesema Dkt. Samia.
Benki ya NMB imekabidhi gawio la shilingi bilioni 45.5 ambapo serikali inamiliki 31.8% ya hisa katika benki hiyo, huku asilimia zingine zikiwa zinamilikiwa na wadau kutoka sekta binafsi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa kiasi cha gawio ambalo limetolewa na Benki ya NMB ni kikubwa ambacho hakijawai kutolewa na taasisi za serikali.
Dkt. Nchemba amesema kuwa mafanikio ya Benki ya NMB ni taarifa njema katika kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakuwa imara kwa kuongeza chachu katika ukuaji wake.
Amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea na mageuzi katika sekta mbalimbali ikiwemo fedha kutokana na mazingira wezeshe yaliokuwepo.
“Hili lina thibitishwa na Benki ya NMB kupitia gawio la bilioni 45.5 , ulipaji wa kodi, utoaji wa ajira kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa” amesema Dkt. Nchemba.
Amesema kuwa katika bajeti ya mwaka 2023/2024 ya serikali imeweka trilioni moja ambayo inakwenda kutumika kukuza sekta binafsi.
“Wizara ya Fedha inaipongeza Benki ya NMB kwa mafanikio katika kipindi cha miaka 25 na wamekuwa wadau wakubwa kwa kuwa wabunifu na kuendelea kuwa kinara katika kutoa huduma katika sekta ya fedha” amesema Dkt. Nchemba.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna, amesema kuwa katika kuadhimisho miaka 25 ya Mafanikio wametenga Shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kujenga Shule ya Mfano katika eneo na Mkoa ambao atapendekeza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassani kwa ajili ya kuunga jitihada katika sekta ya elimu nchini.
Bi. Zaipuna amesema kuwa lengo ni kuhakikisha sekta ya elimu inapiga hatua na kupata mafanikio.
Amesema kuwa mafanikio ya Benki ya NMB yanapaswa kuendana jamii katika kuhakikisha wanatatua changamoto zilizopo.
Bi. Zaipuna amesema kuwa Benki ya NMB itaendelea kuwa mdau mkubwa wa serikali kwa kufanya uwekezaji nchini kupitia kilimo na biashara.
Amebainisha kuwa wamefanikiwa kutoa mikopo trilioni 5.2 kwa ajili ya wakulima, wafanyabiashara wadogo pamoja na watu binafsi.
“Mwaka huu tumefanya maboresha katika hospital ya Taifa ya Muhimbili katika hodi ya kujifungulia wakina mama kwa kununua vifaa mbalimbali pamoja na vitanda” amesema Bi. Zaipuna.
Naibu Cavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bi. Sauda Msemo, amesema kuwa wanaendelea kutekeleza majukumu yao ikiwemo dhamana ya kusimamia sera na utulivu wa uchumi nchini pamoja kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza uchumi.
Bi. Msemo amesema kuwa serikali kupitia BOT wanaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi kwa gharama nafuu.
Hata hivyo ameipongeza Benki ya NMB kwa jitihada kubwa ambazo wamefanya kwa kuboresho na kufanya mabadiliko na kufanikiwa kuwa na mtaji mkubwa na kutengeza faida.