Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe.Kapenjama Ndile ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kimkoa kwenye viwanja vya Rwinga mjini Namtumbo
Mwanafunzi wa shule ya msingi Namtumbo Amina Said akisoma risala ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Rwinga mjini Namtumbo ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas aliyewakilishwa na Mhe.KapenjamaNdile
Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi za sekondari mjini Namtumbo wakiandamana katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Rwinga mjini Namtumbo
wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mtakatifu Agnes Chipole Songea wakitumbuiza kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa wilayani Namtumbo.
Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi za sekondari mjini Namtumbo wakiandamana katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Rwinga mjini Namtumbo
……………………………………………………
Na Albano Midelo,Namtumbo
WAZAZI wametahadharishwa kuzingatia usalama wa mtoto katika
ulimwengu wa kidijitali kutokana na takwimu hapa nchini kuonesha kuwa
asilimia 67 ya Watoto wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 17 wanatumia
mitandao bila usimamizi.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban
Thomas katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mheshimiwa
Kapenjama Ndile katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika,kimkoa
yamefanyika katika uwanja wa Rwinga mjini Namtumbo.
Kanali Thomas amesema takwimu zinaonesha kuwa katika kila nchi
duniani,Watoto ndiyo kundi linaloongoza kwa utumiaji wa bidhaa za
mawasiliano bila kuzingatia matumizi sahihi.
Amebainisha zaidi kuwa Watoto wengi wanatumia mitandao mbalimbali
ikiwemo simu za ndugu zao,walezi,wazazi na marafiki hivyo ametoa rai
kwa jamii kuhakikisha Watoto wanaelekezwa kuzingatia matumizi sahihi na
salama dhidi ya vifaa vya kieletroniki kutokana na kasi ya uwepo wa
vitendo vya ukatili vinavyofanyika mtandaoni.
Ametoa rai kwa kila mzazi na mlezi kuhakikisha mtoto hatumii vifaa vya
kieletroniki kama simu,intaneti na luninga bila uangalizi wa karibu ili
kumepusha kujiingiza kwenye maeneo hatarishi ya kufanyiwa ukatili wa
mtandaoni.
“Mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine nchini,bado tunakabiliwa na vitendo
vya ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo ubakaji,ulawiti,utumikishaji katika
ajira hatarishi,ndoa na mimba za utotoni’’,alisisitiza.
Hata hivyo Kanali Thomas,amekemea tabia ya baadhi ya wanaume kurithi
wajane na kutelekeza Watoto kwa kuwaacha wanaangaika bila huduma za
msingi ambapo amesema vitendo hivyo vimekithiri na kuendelea kuripotiwa
katika vituo vya polisi,ustawi wa jamii na katika ngazi zote za
kaya,Kijiji,kata,wilaya hadi mkoa.
Ametoa rai kwa viongozi wote wa serikali na madhehebu ya dini kuwajibika
kwa kuwalinda Watoto na kuwapeleka shule,kuwalea na kuwapa haki zao
za msingi kama chakula,matibabu.malezi bora na kuwalinda dhidi ya
unyanyasaji.
Amesema Mkoa wa Ruvuma unaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa
watoto ikiwemo elimu kwa Watoto kuanzia shule za awali,msingi,sekondari
hadi vyuo vikuu na kutoa huduma ya afya zikiwemo chanjo kwa Watoto ili
kuepuka maradhi na kuwa na afya bora.
Awali akisoma risala ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa
Afrika,mwanafunzi wa shule ya msingi Namtumbo Amina Said alisema
maadhimisho hayo yanafanyika kila mwaka Juni 16,kuendeleza
kumbukumbu ya mauaji ya Watoto zaidi ya 600 yaliyofanywa na makaburu
katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya kusini Juni 16,1976.
Watoto hao wa kiafrika waliuawa baada ya kuandamana ili kudai haki zao
za msingi kama vile kutobaguliwa katika mfumo wa kupata elimu,afya na
kunyanyaswa na makaburu.
Hata hivyo katika risala hiyo Watoto hao wameishukuru serikali ya Awamu
ya Sita kwa kiwango kikubwa kuwapatia Watoto wa Tanzania fursa sawa
katika masuala mbalimbali yakiwemo elimu,afya na ulinzi kuanzia ngazi ya
familia,wilaya hadi mkoa
Kauli mbiu ya maadhimisho ya maadhimisho ya siku yam toto wa Afrika
2023 ni zingatia usalama wa mtoto katika ulimwengu wa kidijitali.