Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adama Malima
………..
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adama Malima amesema sekta ya biashara ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi hapa nchini hivyo amewataka wadau wa uchumi kushikamana katika kuweka mazingira ambayo yanavutia wawekezaji ili kuinua uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Adam Malima ametoa kauli hiyo Juni 15 mwaka huu kwenye mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa uliofanyika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema uwepo wa mazingira mazuri ya biashara huvutia wawekezaji na kufanya ukuaji wa pato la Mkoa kutokana na ushuru na kodi mbalimbali zinazokusanywa kutoka kwa wafanya biashara.
“…tuendane na malengo yetu ya kutengeneza mazingira wezeshi, mazuri zaidi ambayo ndiyo msingi wa maelekezo ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan…” amesema Mhe. Adam Malima.
Aidha, amewataka wakuu wa taasisi za umma na binafsi kufanya kazi kwa umoja kwa kuthamini mchango unaotolewa na kila mmoja ili kufanikisha maendeleo ya Mkoa huo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru na Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya kuondoa changamoto za uwekezaji na kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi.
Naye Mkurugenzi wa idara ya masoko kutoka Kampuni ya Sukari Kilombero Bw. Fimbo Butallah amesema wataendelea kudhamini mikutano ya biashara ili kufungua fursa za kiuchumi za Mkoa huo.
Aidha, ameongeza kuwa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kinafanya upanuzi wa kiwanda ili kuongeza uzalishaji wa sukari na kutoa fursa za ajira kwa wananchi wa Mkoa huo. sambamba na kutoa ajira kiwanda kinapata malighafi ya miwa kutoka kwa wakulima 8,000 ambao wanazalisha tani 600,000 za miwa kwa mwaka.
ameongeza kuwa, kupitia upanuzi wa kiwanda hicho watahitaji nyongeza ya wakulima 1,400 ili kufikisha tani 1,500,000 za miwa kwa mwaka na kukidhi mahitaji ya kiwanda hicho.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga Bw. Faustini Almas amezilalamikia Halmashauri za Mkoa huo kwa kile alichodai kutoshirikishwa kwenye masuala yanayowahusu maendeleo ya Mkoa huo.