Dkt. Athuman Kihara, Daktari Bingwa wa magonjwa ya uzazi na wanawake ambae pia ni mkuu wa msafara wa madaktari bingwa waliowasili katika mkoa wa Tabora katika kampeni ya “Madaktari Bingwa wa mama”
Mtaalamu wa usingizi akiendelea na zoezi la kumhudumia mgonjwa katika Kituo cha Afya Uliankuru Mkoani Tabora baada ya kuwapokea madaktari bingwa wa uzazi na wanawake kutoka taifa.
……………………………….
Na Mwandishi wetu – Tabora
Mjamzito ambaye mimba yake ilitunga nje ya via vya uzazi, hali ambayo ilitishia uhai wa mama na mtoto ameokolewa maisha kwa upasuaji na jopo la wataalamu mabingwa, ndani ya Kituo cha Afya Ulyankulu.
Pamoja na mama huyo, wengine waliokuwa na tatizo la uchungu pingamizi na tatizo la kupasuka kizazi nao wamefanyiwa upasuaji pamoja na matibabu mengine.
Jopo lililofanya matibabu hayo linajumuisha daktari bingwa wa akina mama na uzazi, daktari bingwa wa watoto, daktari bingwa utoaji usingizi, muuguzi mkunga na muuguzi bingwa wa watoto wachanga.Lipo mkoani Tabora kwa kambi maalum ya mwezi mmoja kupitia huduma za mkoba mahususi kwa huduma za mama na mtoto iliyoanzishwa na Rais Dkt. Samia Hassan ‘Mama Samia Wavushe Salama Mama Zetu’.
Lengo la huduma hiyo ni kuwajengea uwezo watumishi wa vituo vya ngazi ya msingi ili wawe na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi hatimaye kuokoa uhai wa mama na mtoto.
Akizungumza na waandishi wa habari, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Uzazi na Wanawake Dkt. Athuman Kihara amesema Timu iliyokuja Tabora tulijikita Ulyankulu na Kaliua.
“Wahudumu za afya wote, madaktari wauguzi na hata wa idara nyingine wamepokea kwa ushirikiano mkubwa sana {program hii} kuliko tulivyotegemea.
Ameongeza “Ulyankulu tumepata ushirikiano mzuri, mambo mengi tuliyowashauri wameyafanyia kazi, wameipokea hii kampeni kwa ushirikiano mkubwa sana, kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya na vituo vya afya.
“Tumepeana ujuzi nao wote ambao wanahusika upande wa kumsaidia mama na mtoto wakati wa uzazi. Tulipokuwa Ulyankulu tulipata kesi ya mimba iliyojipandikiza nje ya via vya uzazi.
“Kwa mazingira yao ingekuwa upasuaji mgumu tumefanya nao upasuaji {salama} na kwa wiki zote mbili {walizokuwa huko} mpaka mama anaruhusiwa alikuwa vizuri kabisa.
Amebainisha “Kaliua kuna wakina mama walikuja wamepasuka kizazi, tuliwasaidia na wanaendelea vizuri na wiki iliyopita waliruhusiwa.
“Wakina mama wengine walikuwa na uchungu pingamizi ambapo mama anashindwa kujifungua kwa muda uliokadiriwa, wamefanyiwa upasuaji na wapo salama
Amesema hatua ambayo imewawezesha pia wataalamu wa vituo hivyo kupata ujuzi wa nini kifanyike na namna gani ya kuwaangalia wakina mama wakiwa na hali hizo, ili wasifikie katika hatua hatarishi.
Amesisitiza “Tume-base sana {tumejikita sana} katika wodi ya kujifungulia, NICU {huduma ya uangalizi kwa watoto wanaohitaji uangalizi maalum pamoja na ‘labour ward’.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dkt. Amin Vasomala amesema kambi hiyo imekuwa ya manufaa makubwa.
“Imekuja kwetu kwa ajili ya mafunzo elekezi kwa watumishi wangu imekuwa msaada mkubwa, wameanza Ulyankulu wamefanya vitu vizuri.
“Watumishi wangu wameleekezwa vituoni dawa za kutoa usingizi, uzazi na kuzalisha wamefanya vizuri sana, tunakusudia iwe endelevu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa Kaliua wamesema wanaishukuru Serikali kupeleka jopo la wataalamu hao mabingwa.
“Nimemleta dada yangu kufanyiwa upasuaji, wanaoingia wanatoka salama, tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za afya,” amesema Bahati Jumanne.